Riyadh, Saudi Arabia
Mshambuliaji wa Brazil, Neymar amejiunga na klabu ya Al Hilal ya Saudi Arabia akitokea PSG ya Ufaransa kwa ada inayotajwa kufikia Pauni 77 milioni.
Neymar katika siku za karibuni amekuwa akihusishwa na mipango ya kuihama PSG na Jumamosi aliachwa katika kikosi cha timu hiyo kilichoumana na Lorient katika mechi ya Ligi 1 na kutoka sare ya bao 1-1.
Inaaminika kwamba Neymar mwenye umri wa miaka 31, amechukua uamuzi wa kuachana na PSG baada ya kufahamu kwamba hakuwa katika mipango ya baadaye ya kocha mpya wa timu hiyo, Luis Enrique.
PSG pia inaaminika kuwa katika mkakati wa kuachana na wachezaji wenye majina makubwa na waliosajiliwa kwa bei mbaya, lengo likiwa ni kupunguza gharama kubwa za mishahara.
Hivi karibuni nyota mwingine wa bei mbaya aliyekuwa akiichezea PSG, Lionel Messi aliachana na timu hyo na kutimkia nchini Marekani akiendelea kucheza soka nchini humo.
“Nipo hapa Saudi Arabia, mimi ni wa Hilali,” alisema Neymar katika picha ya video iliyoonekana kwenye mitandao ya kijamii ya klabu hiyo.
Habari zaidi zinadai kwamba akiwa Saudi Arabia na klabu hiyo, Neymar atakuwa akilipwa kiasi cha Pauni 129.2 milioni kwa mwaka, fedha ambazo ni karibu mara sita ya kiasi alichokuwa akilipwa PSG.
“Wakati wote ni vigumu kuagana na mchezaji wa kipekee kama Neymar, mmoja wa wachezaji mahiri duniani, sitosahau siku aliyowasili PSG na kile alichochangia katika klabu na mradi wetu kwa miaka sita iliyopita,” alisema rais na mtendaji mkuu wa PSG, Nasser Al-Khelaifi.
Neymar ambaye amekuwa akiandamwa na maumivu ya enka mara kwa mara, hadi anaondoka PSG ameichezea timu hiyo mara 173 na kuisaidia kubeba mataji 13 yakiwamo matano ya Ligi 1 pamoja na kuiwezesha kufikia fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2020.