Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji, Francis Baraza (pichani) amesema kwenye dirisha hili la usajili anatarajia kuimarisha kikosi chake kwa kusajili wachezaji wawili kwenye eneo la ushambuliaji na ulinzi.
Baraza ambaye amejiunga na Dodoma akichukua nafasi ya Melis Medo ambaye alioneshwa mlango wa kutokea na walima zabibu hao.
Kocha huyo alisema Ligi Kuu NBC ni ngumu, imekuwa bora zaidi na amekiona kikosi chake kinavyocheza, atakachokifanya ni kuboresha kikosi kwa kuongeza wachezaji kadhaa.
“Maeneo ambayo nitaenda kuongeza nguvu ni mmoja kwenye eneo la ushambuliaji, nilionao (washambuliaji) hawatoshi hivyo natakiwa kuongeza mmoja ambaye atakuja kuongeza kitu kwenye kikosi cha kwanza.
“Lakini pia kwenye eneo la ulinzi natakiwa kuongeza beki mwingine kwa wale waliopo vimo vyao sio vikubwa, ni wafupi hivyo natakiwa kuangalia mlinzi mwenye kimo aje kuongeza nguvu kikosini,” alisema Baraza.
Alisema kuwa ligi kuu inazidi kuwa ngumu hivyo ili atimize malengo waliyojiwekea kama timu lazima wawe na kikosi bora chenye ushindani mkubwa ndio maana ameamua kuingia sokoni kusaka nyota wawili.
