Na mwandishi wetu
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) leo Jumanne limetangaza kuusogeza mbele mchezo wa hatua ya nusu fainali wa Kombe la FA (ASFC) kati ya wenyeji Singida Big Stars dhidi ya Yanga uliokuwa upigwe Mei 7, mwaka huu kwenye Uwanja wa Liti, Singida.
Hiyo ni baada ya uongozi wa Yanga, kuomba mchezo huo usogezwe mbele ili kutoa muda wa kuiandaa timu yao kwa ajili ya mchezo wa mkondo wa kwanza wa nusu fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Marumo Gallants ya Afrika Kusini, mechi itakayopigwa Mei 10 kwenye
Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
TFF imeeleza kuwa imeusogeza mchezo huo baada ya kupokea barua ya maombi ya kusogezwa mbele na sasa utapangiwa tarehe nyingine.
Yanga iliomba mchezo huo kusogezwa mbele kwa kuwa baada ya mchezo huo timu yao ingekosa muda wa kujiandaa na mechi ya Marumo kutokana na safari ya kutoka Singida hadi Dar es Salaam ambako ndipo mchezo huo utachezwa.
“Tumepokea maombi ya Yanga na tumeona yana tija ukizingatia haya ni mashindano ya kimataifa na Yanga ndio mwakilishi pekee kwa hiyo tumekubali ombi lao na tunawatakia maandalizi mema ili waweze kufanya vizuri kwenye mchezo huo,” ilieleza sehemu ya taarifa iliyowekwa mtandaoni na TFF.
Kufuatia mabadiliko hayo TFF pia imeusogeza mbele mchezo wa nusu fainali ya kwanza ya Kombe la FA kati ya Simba na Azam FC uliokuwa upigwe Mei 6 na sasa utachezwa Mei 7, mwaka huu lengo likiwa ni kuzipa nafasi timu hizo kujiandaa vyema kwa ajili ya mchezo huo.
Yanga imetinga nusu fainali Kombe la Shirikisho baada ya kuitoa Rivers United ya Nigeria kwa matokeo ya jumla ya mabao 2-0 Jumapili iliyopita.
Soka Mechi ya Yanga, Singida yasogezwa mbele
Mechi ya Yanga, Singida yasogezwa mbele
Read also