Na mwandishi wetu
Baada ya jana Jumanne kulala kwa mabao 2-1 dhidi ya Ihefu FC, kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi, amesema ugumu wa ratiba ya Ligi Kuu NBC umechangia kupoteza mchezo huo na kuvunja rekodi yao ya kutopoteza mechi tangu mwaka 2021.
Yanga ilipoteza mechi hiyo kwenye Uwanja wa Highland Estate, Mbeya na kushindwa kufikia rekodi ya kutopoteza mechi 50 kwenye ligi. Mara ya mwisho Yanga ilipoteza mechi Aprili 2021 kwa kufungwa na Azam bao 1-0, bao lililowekwa kimiani na Prince Dube.
Akizungumza baada ya mchezo Nabi aliwapongeza Ihefu kwa ushindi kwani walistahili matokeo hayo, walikuwa bora uwanjani na nidhamu yao ya mchezo ilikuwa nzuri.
“Hatukucheza vizuri, nidhamu yetu ya mchezo haikuwa nzuri, miili ya wachezaji ina uchovu mkubwa kuna wakati walikuwa hata wazito kukimbia.
“Ratiba imekuwa ngumu sana kiasi cha kuchosha wachezaji, tumecheza takribani mechi nane ndani ya mwezi mmoja na tunasafiri sana, muda mwingi ni mazoezi si ya kujenga miili na mifumo kutokana na muda,” alisema Nabi.
Aidha, alisema wakati mwingine ni vyema kupoteza mechi baada ya kutofungwa kwa muda mrefu ili kuirudisha akili katika mfumo wa upambanaji akimaanisha kutofungwa muda mrefu pia huchangia kuleta presha.
Kocha Mkuu wa Ihefu, Juma Mwambusi alisema anamshukuru Mungu kwa kupata matokeo hayo japo aliwaambia wachezaji wake waiheshimu Yanga maana ni mabingwa wa kihistoria, wanaongoza ligi, timu kubwa ambayo haijafungwa ila waingie uwanjani wakacheze mpira.
“Kila jambo lina wakati wake, nimeikuta timu katikati tunapoteza michezo, kikubwa nilichofanya nilirekebisha baadhi ya mambo, walikuwa wanapoteza mechi kwa kutotumia nafasi lakini nilikaa na wachezaji muda mrefu nikawaambia tunaweza kufanya kitu.
“Pia niliwaambia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo kuwa hakuna timu iliyocheza mechi 50 bila kupoteza dunia nzima, sisi tutaivunja rekodi hii, vijana wakanielewa nikawaambia tukiingia uwanjani tujiamini kitu cha kwanza lakini pia tutumie nafasi tutakazopata,” alisema Mwambusi.
Pamoja na matokeo hayo, Yanga iliyocheza mechi 13 imeendelea kusalia kileleni kwa pointi 32 sawa na Azam inayoshika nafasi ya pili kwa mechi 14 lakini ikizidiwa kwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa. Simba ni ya tatu kwa pointi 31 baada ya mechi 14.
Soka Nabi adai ratiba imewaponza
Nabi adai ratiba imewaponza
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
