Na mwandishi wetu
Baada ya tetesi za hapa na pale hatimaye habari mbili zimeibuka kuhusu mshambuliaji wa Simba, Bernard Morrison. Moja ni ya kupumzishwa hadi mwishoni mwa msimu wakati mkataba wakeutakapofikia mwisho.
Habari hiyo inabebwa na habari ya pili ambayo inaonekana kuwa na nguvu zaidi kuwa Simba imeamua inaachana na mchezaji huyo na ilichofanya ni kuchelewesha tu jambo hilo hadi baada ya kumalizika mkataba Hiyo maana yake ni kwamba akimaliza mapumziko na mkataba umekwisha. Ni kama vile ameachwa kiaina ili suala hilo limalizike kimya kimya bila makeke hasa kwa kuwa zipo habari kwamba anaelekea kwa mahasimu wao Yanga.
Na ingawa bado haijathibitishwa lakini vyanzo mbalimbali vimekuwa vikieleza kuwa Simba imeamua kuachana na mchezaji huyo kutokana na vitendo vyake vya utovu wa nidhamu lakini pia inadaiwa ni baada ya kumalizana na Yanga kwa ajili ya kuitumikia timu hiyo msimu ujao.
Kabla ya taarifa hiyo iliyotolewa leo kupitia mitandao ya kijamii ya Simba, tayari kuliibuka sintofahamu kuhusu hatma ya mchezaji huyo ambaye mara ya mwisho alionekana akiitumikia Simba kwenye mchezo dhidi ya Yanga ulioisha kwa suluhu kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Simba kupitia taarifa yake ilieleza kuwa inamshukuru Morrison raia wa Ghana kwa mchango wake katika kipindi cha miaka miwili aliyoitumikia timu hiyo ikiwemo kuwapa ubingwa wa Ligi Kuu Bara, Kombe la Mapinduzi, Kombe la Shirikisho la Azam na Kombe la Mapinduzi.
“Klabu yetu imempa mapumziko ya hadi mwisho wa msimu mchezaji Bernard Morrison. Simba imefikia maamuzi hayo baada ya pande zote mbili kukubalina kwa lengo la kumpa nafasi Morrison kupumzika na kushughulikia mambo yake binafsi.
“Simba inamshukuru Morrison kwa mchango wake kwa kipindi chote alichohudumu ndani ya klabu yetu. Kwa mchango na mafanikio hayo klabu inamshukuru mchezaji huyo kipenzi cha Wanasimba kwa kujitoa kwake kuipigania klabu yake.
“Simba inamtakia kila la heri Morrison katika mapumziko yake na safari yake ya soka hapo baadaye,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Habari ya Morisson imekuja wakati jana kwenye mitandao ya kijamii kulikuwa na video iliyomuonyesha mchezaji huyo akiwa na kipa Aishi Manula ambapo kwenye video hiyo, Morrison alikuwa akisema, ‘bado nipo sana,’ alikuwa akifundishwa kutamka maneno hayo na Manula.
Taarifa nyingine ya Morisson iliyopatakana kwenye mitandao leo, inamnukuu mchezaji huyo akisema kwamba atakosekana katika klabu hiyo kwa kipindi cha msimu kilichobaki kwa sababu ya matatizo ya kifamilia ambayo yataathiri uwajibikaji wake katika timu iwapo ataendelea kuitumikia katika mechi zilizobaki.
Katika taarifa hiyo Morrison ameitakia kila lakheri Simba kwa michezo iliyobaki huku akiomba amalize matatizo yanayomkabili ili aweze kurudi na kuitumikia Simba kwa mechi zilizobaki.
Morrison alitua nchini mara ya kwanza mwaka 2020 na kusaini Yanga alikodumu kwa miezi sita kabla ya baadaye kutimkia Simba ambako amehudumu kwa miaka miwili, mkataba wake ukitarajiwa kufikia ukingoni mwishoni mwa msimu huu.
Soka Simba yaachana na Morrison
Simba yaachana na Morrison
Read also