London, England
Klabu ya Crystal Palace imedai kuwa dhana ya uadilifu kwenye michezo imekosa maana baada ya Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa) kuipora timu hiyo nafasi ya kushiriki Europa Ligi na kuishusha hadi kwenye michuano ya Uefa Conference Ligi.
Baada ya kushinda Kombe la FA msimu uliopita, Palace walifuzu kucheza Europa Ligi lakini waliadhibiwa kwa kuvunja kanuni ya Uefa inayohusu umiliki wa klabu zaidi ya moja kwa mtu mmoja.
Klabu hiyo hata hivyo ilikata rufaa CAS lakini uamuzi wa CAS uliotangazwa Jumatatu hii Agosti 11, 2025 unamaanisha kwamba Palace sasa watacheza Uefa Conference Ligi.
Katika taarifa yake kuhusu uamuzi huo, Palace walisema wanaona haitowezekana wao kusikilizwa kwa haki na wanauona uamuzi huo kuwa ni kielelezo cha kukosekana uadilifu katika michezo.
Kwa mujibu wa Palace uamuzi huo unaonesha jinsi baadhi ya klabu, taasisi na watu binafsi walivyo na hadhi na nguvu za kipekee.
“Kukua kwa mambo haya yasiyo na afya yameathiri matumaini na ndoto za mashabiki wa Crystal Palace na timu nyingine Ulaya kote katika kushindana na kusonga mbele na adhabu zinatolewa katika namna isiyo sahihi,”ilieleza taarifa ya Palace.
Klabu hiyo hata hivyo iliahidi kuendelea kufanyia kazi ushauri wa kisheria kwa ajili ya hatua zinazofuata wakati huu wakijiandaa kushiriki Conference Ligi.
Michuano ya Conference Ligi ni ya tatu kwa ukubwa kwa ngazi ya klabu barani Ulaya baada ya Ligi ya Mabingwa na Europa Ligi.
Klabu ya Nottingham Forest ambayo msimu uliopita ilimaliza nafasi ya saba katika Ligi Kuu England imepandishwa kucheza Europa Ligi ikichukua nafasi ya Palace.
Awali Palace walipewa muda hadi Machi Mosi mwaka huu kuonesha kwa Uefa jinsi mfumo wao wa umiliki wa klabu ulivyo hasa hoja ya mmiliki mmoja kuwa na hisa nyingi katika klabu nyingine lakini hadi siku hiyo inapita hawakuweza kuliweka jambo hilo wazi.
Tatizo lilianzia kwa kampuni ya Eagle Footballing Holdings Limited inayomilikiwa na mfanyabiashara wa Marekani John Textor, kampuni ambayo ina hisa katika klabu ya Lyon ya Ufaransa na asilimia 43.9 ya hisa katika klabu ya Palace.
Katika utetezi wao, Palace walidai kuwa, Textor hana maamuzi katika uendeshaji kwenye klabu ya Palace.
Hoja hiyo ilikataliwa kwa madai kuwa kanuni zinakataa muingiliano wa aina hiyo ambao unampa nafasi mtu kuwa na ushawishi kwa kuwa na hisa zaidi ya asilimia 30 ya hisa zote kwenye klabu zaidi ya moja.
