Na mwandishi wetu
Yanga imeendeleza ubabe katika Ligi Kuu NBC baada ya kuichapa Prisons mabao 2-1 na kuendelea kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Jumapili hii kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, Yanga walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya nane mfungaji akiwa Clement Mzize ambaye aliitumia vizuri pasi ya Pacome Zouazoua.
Bao hilo liliongeza kasi ya mchezo kwa timu zote kupambana, Yanga wakisaka bao la kuongeza wakati Prisons waliokuwa wenyeji wa mchezo huo wakipambana kusaka bao la kusawazisha.
Katika mapambano hayo walikuwa ni Yanga ambao juhudi zao zilizaa matunda kwa kuandika bao la pili lililofungwa dakika ya 45 na Zouzoua akiitumia vizuri pasi ya beki Yao Kouassi.
Prisons hata hivyo mabao hayo hayakuwakatisha tamaa, waliendelea kupambana kipindi cha pili na juhudi zao kuzaa matunda dakika ya 63 walipopata bao lao pekee lililofungwa na Jeremiah Juma.
Juma alifunga bao hilo kwa mpira wa adhabu ambayo ilitolewa na mwamuzi Ahmed Arajiga baada ya kipa wa Yanga, Metacha Mnata kumchezea rafu Samson Mbagula nje kidogo ya eneo la penalti.
Kwa kosa hilo Yanga ilijikuta ikipata pigo na kubaki 10 uwanjani baada ya kipa huyo kupewa kadi nyekundu na mwamuzi hali iliyomfanya kocha Miguel Gamondi kumtoa Farid Mussa na nafasi yake kuingia kipa Aboutwalib Mshery.
Ushindi huo sasa umeifanya Yanga kuongoza ligi ikiwa na pointi 40 katika mechi 15 ikiwa imeiacha Azam FC inayoshika nafasi ya pili kwa tofauti ya pointi nane.
Yanga pia imwaacha mahasimu wake Simba wanaoshika nafasi ya tatu kwa tofauti ya pointi 10, Simba ina pointi 30 katika mechi 13 ilizocheza hadi sasa.
Katika mechi nyingine za ligi hiyo zilizochezwa Jumapili hii, Tabora United ilitoka sare ya bao 1-1 na Namungo wakati Dodoma Jiji na Mashujaa nazo zilitoka uwanjani kwa sare kama hiyo.
Soka Yanga yaendeleza ubabe ligi kuu
Yanga yaendeleza ubabe ligi kuu
Read also