Manchester, England
Kocha wa Man City, Pep Guardiola amempongeza mshambuliaji wake Erling Haaland akisema bao la ushindi alilofunga dhidi ya Borussia Dortmund Jumatano usiku katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya limemkumbusha ubora wa Johan Cruyff na Zlatan Ibrahimovic au Ibra.
Haaland aliifungia City bao la pili wakati timu hiyo ikitoka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Dortmund, timu ya zamani ya Haaland, alipouwahi mpira wa juu na kujaza wavuni kwa mguu wa kushoto. Hilo ni bao la 13 kwa Haaland msimu huu ambao ni msimu wa kwanza kwake tangu ajiunga na City akitokea Dortmund na linatajwa kuwa ndilo bao bora kati ya yote aliyofunga hadi sasa akiwa na City.
Akizungumzia bao hilo, Pep alisema kwamba linamkumbusha Cruyff na Ibrahimovic ambaye katika hali ya utani Pep alimwita ‘rafiki’ baada ya wawili hao kuwa na ugomvi wakati wakiwa pamoja katika klabu ya Barcelona, Pep akiwa kocha na Ibrahimovic mchezaji.
“Labda wanaonijua wanajua vyema ushawishi wa Johan Cruyff katika maisha yangu binafsi, alikuwa kiongozi na mshauri wangu, miaka mingi iliyopita alifunga bao la aina yake pale Nou Camp katika mechi dhidi ya Atletico Madrid, ni ‘jambo zuri, Erling amefanya kama Cruyff,” alisema Pep na kumtaja Cruyff ambaye mbali na kuwa mchezaji, pia aliwahi kuwa kocha Barcelona wakati Pep akiwa mchezaji.
“Mara tu baada ya Erling kufunga bao nilifikiria na kuona hali ya kufanana, nimemkumbuka rafiki yangu Ibrahimovic ambaye pia alikuwa na uwezo wa kuupeleka mguu hewani na Erling naye katika hilo yuko hivyo hivyo,” alisema.
“Nafikiri hivyo ndivyo alivyo kimaumbile, ni mwepesi, ananyumbulika na baada ya kuonekana ana uwezo wa kuupeleka mpira kwenye nyavu, nafikiri mama na baba yake walimsaidia kwa kumfanya awe mwenye kunyumbulika.”
Katika mechi hiyo, Dortmund ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao mfungaji akiwa Jude Bellingham aliyeujaza mpira wavuni kwa kichwa muda mfupi baada ya mapumziko kabla ya City kusawazisha kupitia kwa John Stones na hatimaye Haaland akamaliza shughuli kwa bao lake tamu dakika nne kabla ya mpira kumalizika.
Haaland aliuwahi mpira wa juu uliopigwa na Joao Cancelo na kuusukumiza wavuni kwa guu lake la kushoto, bao ambalo si tu kwamba liliihakikishia timu yake ushindi lakini pia lilikuwa na maana kubwa kwa kocha wake.
Kwa Dortmund bao hilo lililofungwa na mchezaji wao wa zamani limewaachia maumivu makubwa hasa kwa kuwa lilipatikana baada ya kufanikiwa kumdhibiti vyema mchezaji huyo kwa dakika takriban 80 za mchezo lakini mambo yakaharibika muda mfupi kabla ya mpira kumalizika.
Kimataifa Haaland amkumbusha Pep vitu vya Cruyff, Ibra
Haaland amkumbusha Pep vitu vya Cruyff, Ibra
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
