Manchester, England
Kocha wa muda wa Man United, Michael Carrick amefanya kile ambacho kimekuwa kikisubiriwa kwa hamu na mashabiki wa timu hiyo, kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Ushindi wa mabao 3-2 ambao Man United imeupata Jumapili Mei 3, 2026 dhidi ya Liverpool si tu ni ushindi mkubwa dhidi ya timu kubwa bali pia umetosha kuwa tiketi ya kushiriki michuano mikubwa na yenye hadhi, yaani Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kobbie Mainoo ambaye ndio kwanza ametoka kuongeza mkataba na timu hiyo, ndiye aliyefunga bao la tatu na la ushindi na hivyo kuifanya timu hiyo ibebe pointi tatu muhimu na ikate tiketi ya ligi hiyo kubwa.
Man United licha ya kuanza mchezo huo vizuri kwa kupata mabao mawili yaliyofungwa na Matheus Cunha na Benjamin Sesko na kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 2-0 mambo kidogo yalibadilika kipindi cha pili.
Kipindi cha pili Man United walishindwa kulinda mabao yao na kuruhusu nyavu zao kutikiswa na Dominik Szoboszlai na Cody Gakpo ingawa Mainoo alifuta makosa hayo kwa kuifungia timu yake bao la tatu na la ushindi.
Baada ya kuzikosa fainali za Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa misimu miwili, hatimaye wababe hao wa soka wamerudi kwa kishindo katika michuano hiyo mikubwa na yenye hadhi yao.
Kwa Carrick ambaye ndio kwanza ana miaka 44, ushindi huu ulioirudisha timu hiyo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya ni kete nyingine muhimu tangu akabidhiwa timu hiyo Januari mwaka huu.
Carrick tangu akabidhiwe timu, rekodi yake inaonesha kuwa ameshinda mechi 10 kati ya 14 na sasa kinachojadiliwa ni mambo yake ya baadaye ikiwamo kuaminiwa na kuwa kocha wa kudumu.
Mjadala huo hata hivyo haumsumbui Carrick, mara kadhaa amenukuliwa akisema kwamba suala hilo halipo katika fikra zake badala yake wakati wote anaangalia namna ya kuzikabili changamoto zilizo mbele yake.
Kimataifa Man Utd yafuzu Ligi ya Mabingwa
Man Utd yafuzu Ligi ya Mabingwa
Read also
