London, England
Bondia Anthony Joshua amefanikiwa kumchapa Robert Helenius kwa KO ya raundi ya saba, katika pambano la uzito wa juu lililofayika kwenye Ukumbi wa O2 London, usiku wa kuamkia leo Jumapili.
Katika pambano hilo awali ilikuwa vigumu kutabiri nani angeibuka mshindi kwa namna mabondia hao walivyolianza pambano kabla ya Joshua kumsukumizia Helenius ngumi moja kali iliyomuangusha chini.
Kwa ushindi huo Joshua sasa anajiandaa kwa pambano linalosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa ngumi duniani dhdi ya bondia Deontay Wilder, pambano ambalo limepangwa kufanyika Januari mwakani.
Akiuzungumzia ushindi wake kwa Helenius, Joshua alisema ngumi ni mchezo unaokutaka mwenye kubadilika. “Unalazimika kubadili mazingira, ni lazima uwe katika uhalisia huo ili usiwahiwe, nimemaliza kazi yangu usiku huu.”
Katika hali ambayo iliibua hofu kidogo, mara baada ya kipigo hicho Helenius alihitaji kuwekewa oxygen kidogo wakati akiwa chini lakini muda mfupi baadaye akawa sawa na kusimama mwenyewe bila ya msaada wa mtu yeyote na kisha akampongeza Joshua kwa ushindi.
Helenius ambaye ni bondia kutoka Finland, alilazimika kupigana na Joshua baada ya mpinzani wa awali, Dillian Whyte wa Uingereza kuamua mwenywe kujitoa mara baada ya kufanyiwa vipimo.
Baada tu ya kuanza kwa pambano hilo katika sekunde chache za mwanzo alikuwa ni Helenius aliyewahi katikati ya ulingo na kumsukumizia Joshua ngumi ya mkono wa kushoto ambayo hata hivyo haikuwa na madhara kwa Joshua.
Mabondia hao baada ya hapo walikuwa wakicheza kwa kuogopana, hakuna ngumi zozote za maana walizorushiana jambo ambalo pia lilionekana kuwakera mashabiki ambao baadhi yao walianza zomeazomea wakitaka kuona ngumi za uhakika zinapigwa badala ya kuogopana na kuviziana.
Katika raundi ya nne, Joshua alionekana kama kuwatuliza mashabiki aliporusha ngumi ya nguvu ya mkono wa kushoto ambayo ilimrudisha nyuma mpinzani wake lakini hakuonekana kusumbuliwa sana na ngumi hiyo.
Akionekana mwenye kujiamini, katika raundi ya tano, Helenius alianza kumrushia ngumi za hapa na pale Joshua na kushangiliwa na baadhi ya mashabiki.
Ngumi za haraka za raundi ya saba na moja ya nguvu ya mkono wa kulia ndizo zilizomlambisha sakafu Helenius na hapo hapo mwamuzi Victor Loughlin kuamua kumaliza pambano kabla ya kumtangaza Joshua kuwa mshindi.