Rabat, Morocco
Ndoto ya timu ya soka ya vijana chini ya miaka 17 ya Tanzania, Serengeti Boys, kutwaa Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon-17) zimeyeyuka baada ya kulala kwa penalti 4-2 mbele ya Senegal.
Katika mechi hiyo iliyochezwa Jumanne Juni 2, 2026 kwenye Uwanja wa Moulay El Hassan mjini Rabat, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 kabla ya kuingia kwenye mikwaju ya penalti.
Serengeti ndio waliouanza mchezo huo kwa kasi na mapema dakika ya saba waliandika bao mfungaji akiwa ni Hamis Chenga aliyemchungulia vyema kipa wa Senegal kabla ya kupiga shuti lililokwenda upande wa kushoto wa kipa huyo aliyeishia kuutazama mpira.
Senegal au The Young Lions of Teranga walisawazisha bao hilo dakika ya 64 mfungaji akiwa ni Ibrahima Dione aliyemalizia mpira wa adhabu uliopigwa na Souleymane Faye na kipa wa Serengeti, Haji Abdullah kushindwa kuumiliki mpira.
Juhudi za kila timu kupambana kusaka bao la kuongeza hazikuweza kuzaa matunda na ndipo utaratibu wa penalti ulipochukua nafasi yake.
Kwa upande wa Senegal waliofunga penalti zao ni Faye, Sadio, Dione na Thior wakati kwa Serengeti waliofunga ni Yusuph na Mbegelendi huku Klendemo na Mbegu wakikosa.
Hilo linakuwa taji la pili kwa Senegal wakati kwa Serengeti Boys ambao ni mara ya kwanza kufikia hatua ya fainali wameshindwa kutimiza ndoto ya kulibeba taji hilo kwa mara ya kwanza na sasa wanajiandaa kushiriki fainali za Kombe la Dunia.
Kimataifa Senegal bingwa Afcon-17, Serengeti Boys yakwama
Senegal bingwa Afcon-17, Serengeti Boys yakwama
Related posts
Read also
