Na mwandishi wetu
Vinara wa Ligi Kuu NBC, Yanga wamepangwa kundi moja na mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Ahly ya Misri huku wapinzani wao, Simba wakipangwa na Wydad AC ya Morocco.
Yanga iliyo Kundi D katika michuano hiyo mikubwa ya klabu Afrika, imepangwa na timu nyingine za CR Belouizdad ya Algeria na Medeama ya Ghana.
Simba wao wamepangwa Kundi B kwenye droo hiyo iliyochezeshwa jijini Johannesburg, Afrika Kusini pamoja na timu nyingine za Asec Mimosas na Jwaneng Galaxy ya Botswana.
Simba inakutana na timu zote ikiwa inazifahamu kutokana na kukutana nazo hivi karibuni katika michuano ya klabu Afrika.
Msimu uliopita ilipambana na Wydad kwenye robo fainali ya Ligi ya Mabingwa na kufungwa kwa matuta 4-3 baada ya kila timu kushinda bao 1-0 nyumbani kwake.
Lakini pia ilifurushwa na Jwaneng kwenye hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa kwa matokeo ya jumla ya mabao 3-3 misimu miwili iliyopita.
Jwaneng ilisonga kwa faida ya mabao ya ugenini baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-0 nyumbani kwao kabla ya ushindi wa mabao 3-1 kwenye uwanja wa ugenini.
Vilevile, msimu wa 2021-22 ilikutana na Asec kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika na kufungwa mabao 3-0 kwenye mechi ya awali kabla ya kupata ushindi wa mabao 3-1 nyumbani.
Yanga iliyotinga hatua hiyo baada ya miaka 25, ina kumbukumbu ya kuondoshwa kwenye michuano hiyo kwenye hatua ya awali na Ahly baada ya kufungwa jumla ya mabao 3-2 na kudondokea Kombe la Shirikisho, ikipangwa kundi moja na Medeama.
Rekodi zinaonesha, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam kabla ya Medeama kuichapa Yanga mabao 3-1 kwenye mechi ya nyumbani kwao mwaka 2016.
Makundi mengine ya michuano hiyo ni Kundi A linaloundwa na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Pyramids (Misri), TP Mazembe (DR Congo) na FC Nouadhibou (Mauritania). Kundi C lina timu za ES Tunis ya Tunisia, Petro Luanda (Angola), Al Hilal (Sudan) na Etoile du Sahel (Tunisia).
Mechi za kwanza za hatua hiyo zinatarajia kupigwa kati ya Novemba 24 na 25 wakati mechi za pili ni kati ya Desemba 1 na 2, mechi za tatu zitakuwa kati ya Desemba 8 na 9 huku mechi za nne zikipigwa Desemba 19. Mechi za tano itakuwa Desemba 23 na 24 na mechi za mwisho ni Machi 1 na 2, mwaka huu.