Na mwandishi wetu
Uongozi wa Klabu ya Simba umesema maandalizi mazuri ya timu yao yanawapa matumaini ya kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuwafunga Power Dynamos keshokutwa Jumapili.
Katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliochezwa Ndola, Zambia timu hizo zilitoka sare ya kufungana mabao 2-2, hivyo katika mchezo huo wenyeji Simba wanapewa nafasi kubwa ya kushinda.
Mwenyekiti wa timu hiyo, Murtaza Mangungu (pichani juu) alisema kucheza nyumbani na ukomavu wa timu yao kwenye michuano hiyo ndivyo vinampa jeuri ya kushinda mchezo huo ambao wameupa uzito mkubwa mno.
“Niwaambie tu tutashinda mechi ya keshokutwa na tutafuzu makundi na tutafikia malengo yetu ambayo ni kucheza nusu fainali tukiwa hivyo hivyo hatuna furaha, tunachotaka ni kupata matokeo mazuri na mafanikio siyo kufanya maonesho,” alisema Mangungu.
Alisema Simba imeshakuwa timu kubwa Afrika, ndio maana ipo kwenye orodha ya nane bora hivyo hawawezi kukwamishwa na Power Dynamos timu ambayo ndio inapambana kufikia mafanikio yao.
Mangungu amewatoa hofu mashabiki wao akiwataka kwenda kwa wingi uwanjani Jumapili ili kushuhudia namna watakavyoendeleza rekodi yao ya kucheza hatua ya makundi wakiwa kwenye uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.