Rabat, Morocco
Shirikisho la Soka Morocco (FRMF) limetangaza kuachana na kocha wa timu ya Taifa, Vahid Halilhodzic ikiwa ni miezi mitatu kabla ya kuanza kwa fainali za Kombe la Dunia.
Uamuzi huo wa FRMF unadaiwa kutokana na kutokubaliana kati ya shirikisho hilo na kocha huyo kuhusu maandalizi ya timu hiyo maarufu Atlas Lion kwenye fainali hizo. “Pande mbili zimekubaliana kuachana,” ilieleza sehemu ya taarifa ya FRMF.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 69, alianza kuinoa timu hiyo mwaka 2019 na kuiongoza kwenye fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) mapema mwaka huu nchini Cameroon na baada ya hapo aliiwezesha kufuzu fainali za Kombe la Dunia.
Halilhodzic, kocha kutoka Bosnia, kuondoka kwake kunaacha maswali ya nini hasa kimejificha katika uamuzi huo licha ya FRMF kudai kwamba pande mbili zimekubaliana baada ya kutofautiana kuhusu maandalizi ya timu hiyo lakini inaonekana kama kuna zaidi ya hilo.
Kuondoka kwa Halilhodzic huenda ikawa mwanzo mpya kwa winga wa Chelsea, Hakim Ziyech kurudi katika timu ya Taifa ya Morocco baada ya wawili hao kutofautiana na Ziyech kuamua kuachana na timu ya taifa hata alipoitwa kwenye mechi ya kirafiki na DR Congo hakuwa tayari kujiunga na sasa baada ya kocha huyo kuondoka huenda mchezaji huyo akabadili msimamo.
Halilhodzic ni kocha mzoefu wa timu za taifa kwani hapo kabla amewahi kuzinoa timu za Ivory Coast na Japan lakini kote amejikuta akifukuzwa kazi katika mazingira ya kushangaza hasa wakati timu hizo zikijiandaa kwa fainali za Kombe la Dunia baada ya kuziongoza hadi kufuzu.
Kimataifa Morocco yamtimua kocha
Morocco yamtimua kocha
Read also