Na mwandishi wetu
Timu ya Singida Big Stars imezidi kujiimarisha kuelekea msimu ujao baada ya kumsajili Paul Godfrey ‘Boxer’ aliyekuwa akikipiga Yanga SC huku ikitamba kuwa ndiyo kwanza imeanza kushusha silaha zake.
Boxer ambaye Yanga amekuwa akipata changamoto ya nafasi dhidi ya Shaban Djuma na Kibwana Shomari wanaomudu vyema nafasi hizo, amesajiliwa Singida kwa kandarasi ya miaka miwili.
Huyo anakuwa mchezaji wa tatu kutambulishwa na Singida mpaka sasa tangu wapande kushiriki Ligi Kuu ya NBC msimu ujao.
Wengine ni kiungo mkabaji Aziz Andabwile aliyeonesha uwezo mkubwa msimu uliopita akiwa na Mbeya City na Habibu Kyombo kutoka Mbeya Kwanza ambaye awali alikuwa akitajwa kuwaniwa na Simba, ikielezwa walishamalizana kila kitu.
Pamoja na hayo, uongozi wa timu hiyo ambayo awali ilikuwa ikifahamika kama DTB umeeleza kuwa bado hawajamaliza usajili, watatangaza wachezaji wengine watano wapya kuelekea msimu ujao kama ripoti yao ya inavyoainisha.
“Tunataka kujiandaa na kujiweka sawa mapema ndio maana tumekuwa na kasi ya kutambulisha wachezaji wapya, tunataka wafahamu mapema walipo, wazoeane mapema na kazi ianze vizuri kuelekea msimu ujao,” alisema Mtendaji Mkuu wa Singida, Muhibu Kanu.
“Kulingana na ripoti yetu bado inahitajika wachezaji wengine watano, hivyo watu wawe tayari bado hatujamaliza usajili. Tukikamilisha idadi ya wachezaji nane pamoja na hawa watatu ambao tumeshawatangaza hapo tunaweza kutangaza kumaliza zoezi hili,” alisisitiza.
Soka Boxer wa Yanga atua Singida Big
Boxer wa Yanga atua Singida Big
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
