Na mwandishi wetu
Wadhamini wa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Klabu ya Yanga, Shirika la Bima la Taifa (NIC), limeahidi kutoa Sh milioni nne kwa mchezaji atakayeshinda tuzo hiyo kuanzia mwezi huu wa Oktoba.
Wachezaji ambao wameteuliwa kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho ni beki wa kati Dickson Job na viungo washambuliaji, Max Zengeli na Stephan Aziz Ki.
Akizungumza kwenye hafla fupi iliyofanyika mwishoni mwa wiki ya kutangaza zawadi hizo, Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe alisema kiasi hicho cha fedha kilichowekwa na NIC kitaongeza ari ya upambanaji kwa wachezaji wao na kupata matokeo chanya katika mashindano mbalimbali yanayowakabili.
“Milioni nne si kiasi kidogo na Yanga inaweza kuwa ndio klabu ya kwanza kupata mzigo huo na hii inalirahisishia kazi hata benchi la ufundi kwani wachezaji watacheza kwa kujituma mara mbili ya inavyokuwa ili kupata pesa hiyo,” alisema Kamwe.
Alisema zoezi la kupiga kura ili kumpata mshindi linafanyika kupitia mtandao wa klabu hiyo na wahusika wakuu ni mashabiki na wanachama wa timu hiyo.
Naye Msemaji wa NIC, Karimu Meshack alisema tuzo ya mchezaji bora wa NIC Insurance imezingatia vitu vingi ikiwemo ubora wa NIC kama chapa, ubora wa Yanga kwa pamoja na uwepo wa wachezaji wazuri watakaoleta mchuano mkali.
Hii ni mara ya kwanza kwa klabu ya Yanga kupata wadhamini binafsi kwa ajili ya kutoa tuzo ya mchezaji bora wa mwezi baada ya kuingia mkataba wa miaka mitatu na kampuni hiyo wenye thamani ya Sh milioni 900.
Soka Mchezaji bora Yanga kulamba milioni 4
Mchezaji bora Yanga kulamba milioni 4
Read also