Salah mwanasoka bora wa mwaka
Mshambuliaji wa Liverpool, Mohamed Salah ametwaa tuzo ya mwanasoka bora profesheno wa mwaka (PFA), tuzo ambayo pia ameshinda Sam Kerr wa Chelsea kwa upande wa wanawake.
Wawili hao pia walishinda kiatu cha dhahabu kila mmoja kwa kuwa wafungaji bora, kwa Salah kwenye Ligi Kuu England (EPL) na Kerr kwenye Women Super League (WSL) wote kwa msimu wa 2021/22.
Salah sasa anaingia katika rekodi ya wachezaji sita waliowahi kutwaa mara mbili tuzo za PFA akiwa ametanguliwa na wakali wengine wa zamani kina Mark Hughes, Alan Shearer, Thierry Henry, Gareth Bale pamoja na Kevin de Bruyne.
Katika EPLmsimu huu, Salah ameifungia Liverpool mabao 24 akiwa amefungana na nyota wa Korea Kusini, Son Heung-min anayeichezea Tottenham huku Liverpool ikilikosa taji la ligi hiyo mbele ya Man City kwa tofauti ya pointi moja lakini wamefanikiwa kutwaa taji la Ligi (Carabao) na lile la FA huku Salah akiwa na asisti 14.
“Nina chumba changu chenye tuzo na makombe niliyoshinda kwenye kabati na nahakikisha nina nafasi kwa ajili ya tuzo nyingine, wakati wote naacha nafasi na kujaribu kufikiri kwamba mataji yataendelea kuja,” alisema Salah.
Kwa upande wa Kerr wa Chelsea ni raia wa kwanza wa Australia kushinda tuzo hiyo akiwa ameifungia timu ya wanawake ya Chelsea mabao 20 katika WSL na kuiwezesha kutwaa mataji mawili.
“Ni heshima kubwa inapotokea unapigiwa kura na wenzako, nafikiri hiyo ni heshima kubwa mno kwa mchezaji,” alisema Kerr.
Liverpool pia imetoa wachezaji sita wa timu ya EPL kama ifuatavyo; Alisson, Alexander-Arnold, Van Dijk, Thiago, Mane na Salah, wengine katika timu hiyo ni Rudiger wa Chelsea, De Bruyne, Silva na Cancelo wa Man City na Ronaldo wa Man United.
