Na mwandishi wetu
Timu ya Simba inatarajia kuondoka kesho Jumanne kuelekea Marrakesh, Morocco kwa ajili ya mechi yao ya tatu ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wydad AC.
Simba ambayo inaingia kambini leo Jumatatu jioni kujiandaa na mchezo huo, inapaa tena baada ya kurejea jana Jumapili alfajiri ikitokea Botswana kukipiga na Jwaneng Galaxy na kuvuna sara ya 0-0 kwenye Uwanja wa Obed Chilume, Francistown.
Akizungumza na GreenSports, meneja habari na mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema kuwa baada ya mapumziko ya siku moja wamerejea tena mazoezini kujiweka sawa wakifahamu mchezo huo ni mgumu licha ya Wydad kupoteza mechi zake mbili za awali za makundi mpaka sasa.
Alisema kikosi hicho kinaondoka kesho kwa kuwa wanatarajia kutua Morocco keshokutwa Jumatano na watakuwa na siku mbili za kujiandaa kabla ya mchezo wao huo utakaounguruma Desemba 9, mwaka huu, Uwanja wa Marrakesh, mjini Marrakesh kuanzia saa 4.00 usiku.
“Ni mchezo mgumu, Wydad haijapata pointi mpaka sasa nasi tunahitaji ushindi hivyo tunaanza maandalizi leo jioni kuhakikisha tunapigania hilo ugenini na kesho tutaanza safari ya kwenda Morocco maana tunatarajia kufika Jumatano, siku mbili kabla ya mchezo,” alisema Ally.
Katika mchezo wa kwanza wa Kundi B, Simba ilipata sare ya bao 1-1 dhidi ya ASEC Mimosas kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam kabla ya sare nyingine dhidi ya Galaxy, matokeo yanayoifanya timu hiyo ishike nafasi ya tatu ikiwa na pointi mbili.
Wydad inaburuza mkia bila ya pointi baada ya kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Jwaneng nyumbani kisha ikachezea kichapo cha bao 1-0 ilipoumana na ASEC ugenini, na sasa inatafuta ushindi wa kwanza kama ilivyo Simba.
