Rio de Janeiro, Brazil
Rais wa Shirikisho la Soka Brazil, Ednaldo Rodrigues amesema kwamba kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti atakabidhiwa majukumu ya kuinoa timu ya Taifa ya Brazil mwaka 2024.
Brazil ambao ni mabingwa mara tano wa Kombe la Dunia wanaamini kocha huyo Mtaliano atakuwa na timu hiyo kwenye fainali za Copa America Juni mwakani.
Akimzungumzia kocha wa sasa wa timu hiyo, Fernando Diniz, Rodrigues alisema kocha huyo atafanya kazi yake hadi mwaka 2024 wakati huo huo akiendelea na majukumu yake ya sasa katika klabu ya Fluminense.
Tangu kujiuzulu kwa Tite baada ya Brazil kutolewa katika hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia Desemba mwaka jana, timu hiyo haijawa na kocha wa kudumu ambapo hivi karibuni imekuwa ikinolewa na Ramon Menezes katika mechi za kirafiki.
Ancelotti ambaye mkataba wake na Real Madrid unafikia ukomo Juni 2024, kama mpango wa kuinoa timu hiyo utafanikiwa atakuwa kocha wa kwanza asiye raia wa Brazil kuinoa timu hiyo tangu mwaka 1965.
Na ingawa kiongozi mkuu wa soka la Brazil amejiaminisha kuhusu Ancelotti lakini hadi sasa hakujawa na taarifa yoyote rasmi kutoka kwa kocha huyo au klabu ya Real Madrid kuhusu mpango huo japo habari hiyo imekuwa ikizungumzwa kwa takriban miezi sita sasa.
Kimataifa Ancelotti kuanza kibarua Brazil 2024
Ancelotti kuanza kibarua Brazil 2024
Read also