London, England
Wanaharakati za mazingira wa kundi la Just Stop Oil jana Jumatano waliandamana na kufanya vurugu kwenye mashindano ya tenisi ya Wimbledon kwa kuvamia sehemu ya kuchezea na kutupa maganda ya machungwa.
Tukio la kwanza la wanamazingira hao lilitokea wakati wa mechi kati ya Sho Shimabukuro na Grigor Dimitrov hali iliyosababisha mechi hiyo kusimama kwa muda.
Katika tukio la pili wanamazingira hao walisababisha mechi nyingine kati ya Katie Boulter na Daria Saville kusimama kwa muda huku uwanja ikiwa umetapakaa maganda ya machungwa.
Hata hivyo tukio hilo lililoongozwa na waandamanaji wawili walioingia sehemu za kuchezea tenisi halikuchukua muda kwani wana usalama waliwadhibiti na baadaye wachezaji wakasaidia kusafisha uwanja uliotapakaa maganda ya machungwa.
Baadaye taarifa ya polisi ilithibitisha kukamatwa kwa waandamanaji wawili waliokuwa mstari wa mbele mmoja mwanaume na mwingine mwanamke ambao umri wao wote ni miaka zaidi ya 60.
Ulinzi ulikuwa mkali safari hii kuliko mwaka jana ingawa baadhi ya mashabiki wamelalamikia ulinzi huo kwa namna ulivyowachelewesha kuingia uwanjani kwani muda mwingi ulitumika kukagua mashabiki.
Muungano wa kundi la Just Stop Oil linalohusisha wanamazingira wamekuwa wakifanya vurugu katika michezo mbalimbali zikiwamo mechi za soka za Ligi Kuu England pamoja na zile za ligi ya rugby.
Miongoni mwa madai ya wanamazingira wa Just Stop Oil ni pamoja na kuitaka Serikali ya Uingereza iache kutoa leseni mpya katika miradi ya gesi, mafuta na makaa ya mawe.
GreenSports Wanamazingira wavamia mashindano ya tenisi
Wanamazingira wavamia mashindano ya tenisi
Read also
