Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Azam FC, Youssouf Dabo ameeleza kutoridhishwa na mwenendo wa kikosi chake katika mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu NBC.
Azam jana Jumapili ililazimishwa sare ya bao 1-1 na Tanzania Prisons, matokeo ambayo yamefanya tofauti ya pointi kati yao na vinara Yanga kuwa sita huku hiyo ikiwa ni sare ya pili mfululizo baada ya ile ya 0-0 dhidi ya Tabora United.
“Inaumiza kuona unadondosha pointi katika hatua muhimu kama hii ingawa ndio mchezo wa mpira wa miguu ulivyo lakini sifurahishwi kabisa na hiki kitu, kikubwa tunatakiwa kuzidi kupambana ili kurekebisha makosa yetu na kuwaombea mabaya Yanga,” alisema Dabo.
Kocha huyo alisema yeye na wenzake wa benchi la ufundi wataendelea kupambana kwenye uwanja wa mazoezi kurekebisha baadhi ya mapungufu wanayoyaona kwenye mechi zilizopita ili kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye mechi zijazo za ligi.
Alisema kitu kingine kinachowapa tabu ni namna ya kucheza mechi za mikoani ambazo wamekuwa wakikutana na upinzani mkali kiasi kwamba inawapa wakati mgumu kucheza kwenye ubora waliokuwa nao.
Mbali ya kuzidiwa na Yanga kwa pointi na mchezo mmoja lakini timu hiyo ipo mbele kwa tofauti ya pointi moja na michezo miwili dhidi ya Simba iliyopo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi.
Soka Mwenendo Azam haumridhishi Dabo
Mwenendo Azam haumridhishi Dabo
Read also
