Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Geita Gold, Fred Felix Minziro amejiweka kando na timu hiyo baada ya kile kilichoelezwa kuwa ni kushindwana kwa maslahi binafsi nje ya mkataba baina ya pande hizo.
Minziro ameiambia GreenSports leo Jumanne kuwa amekaa kando kutokana na timu hiyo kumkatalia matakwa yake ya kumlipa kiasi cha pesa alichowatajia katika mechi mbili zilizosalia za Ligi Kuu NBC msimu huu.
“Mkataba wangu umeisha tangu Mei 28, niko nje ya mkataba nikijihudumia kwa kila kitu hivyo nikawaambia wanipe pesa kidogo kwa ajili ya kumaliza hizo mechi mbili na siwezi kuwatajia pesa kubwa sababu mimi niko na timu mwaka wa tatu sasa, lakini wakanijibu hawana kiasi hicho.
“Basi mimi nimeondoka zangu, niko Dar es Salaam naendelea na mambo mengine maana kwa tafsiri fupi unaweza kusema hawakutaka labda niendelee kwenye mechi hizi mbili na uzuri nimezungumza nao, tumemalizana vizuri,” alisema Minziro.
Alipotafutwa Ofisa Habari wa Geita, Samwel Dida alisema: “Hizi mechi mbili ziko nje ya mkataba wake, tukamwomba amalizie hizi dakika 180, akatupa utaratibu wake wa malipo, tuliona hatuwezi kumudu na yeye akawa na msimamo wake basi tukamalizana.”
Dida pia alisema mechi zao mbili zilizosalia ikiwemo ya leo dhidi ya Ihefu na ya Mei 9, mwaka huu dhidi ya Mtibwa Sugar, kikosi chao kitakuwa chini ya kocha wa timu ya vijana, Choke Abeid.
Dida aliongeza kuwa kulingana na hali iliyopo sasa baada ya kushindwana na Minziro, imekuwa ngumu kufahamu kama watakua na kocha huyo msimu ujao au la.
