Na mwandishi wetu
Mshambuliaji mpya wa Yanga, Joseph Guede ameugomea uongozi wa timu hiyo kuvaa jezi namba tisa aliyokuwa ameandaliwa na kuichagua namba 14.
Meneja wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe alisema sababu ya kumchagulia namba tisa ni kutokana na uwezo wake wa kufunga kama ilivyo kwa mshambuliaji wao aliyetimkia Pyramids FC ya Misri, Fiston Mayele .
“Amekataa namba tisa ambayo tulimuandalia, badala yake ameichagua namba 14 na sababu kubwa ya kuichagua namba hiyo ni kutokana na kumkubali aliyekuwa mshambuliaji wa zamani wa klabu ya Arsenal na timu ya taifa ya Ufaransa, Thierry Henry,” alisema Kamwe.
Kamwe alisema hawakuwa na namna zaidi ya kukubali ombi lake hilo na amewatahadharisha mabeki na makipa wa timu za Ligi Kuu NBC kujiandaa kwani amemfuatilia mchezaji huyo mazoezini Avic Town na kubaini vyema uwezo wake.
“Guede ni mshambuliaji aliyekamilika kila idara, ana uwezo wa kufunga kwa kichwa na miguu yote miwili, hivyo kwa kupata saini yake tunaamini tumemaliza tatizo la ushambuliaji na kuwafurahisha mashabiki kuhusiana na hilo,” alisema Kamwe.
Taarifa nyingine kutoka ndani ya timu hiyo zinaeleza kuwa kocha mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amempa mshambuliaji huyo wiki mbili za kujiweka sawa kabla ya kuanza kumtumia kwenye mechi za mashindano yote ambayo wanashiriki.
Guede ametua Yanga kuchukua nafasi ya Hafiz Konkoni ambaye kiwango chake kilishindwa kumvutia Gamondi na kuamua kumtoa kwa mkopo kwenye klabu ya Dogan Tûrk Birligi ya Cyprus.