London, England
Kocha wa Chelsea, Mauricio Pochettino (pichani) amekasirishwa kwa namna ambavyo timu yake imekuwa ‘laini’ na kukubali kichapo cha mabao 4-1 mbele ya Newcastle katika mechi iliyochezwa jana Jumamosi.
Katika mechi hiyo ya Ligi Kuu England iliyopigwa kwenye dimba la St James, hadi mapumziko, Chelsea walikuwa tayari wamesawazisha bao moja walilofungwa kabla mambo hayajaharibika kipindi cha pili.
Hali ilikuwa mbaya zaidi kwa Chelsea ambayo ilijikuta ikibaki na wachezaji 10 uwanjani baada ya nahodha wa timu hiyo Reece James kutolewa nje.
Akizungumzia matokeo hayo, Pochettino ambaye alivutiwa na kiwango cha timu yake katika mechi na Tottenham, alisema matokeo ya Newcastle yamemkatisha tamaa kwa kile alichosema timu yake ilishindwa kupambana na kuwa laini.
“Hatukuonesha kwamba tulikuwa tunacheza katika mechi muhimu, tulitakiwa kuwaonesha kwamba mechi ingekuwa ngumu kwao, kwamba isingewezekana kucheza vizuri na kutushinda,” alisema Pochettino.
“Lakini ilikuwa rahisi mno kwa namna ambavyo tulikubali kufungwa, na kwa namna tulivyokuwa laini katika kila eneo la upambanaji,” alisema Pochettino.
“Na hilo ndilo lililonifanya niwe na hasira na kuvurugwa, tunazungumzia kuhusu timu yenye vijana na ni lazima tujifunze lakini nafikiri aina hii ya mechi inanifanya niwe mwenye hasira sana kwa sababu ni suala la kuonesha ubora na upambanaji,” alisema Pochettino.
Matokeo ya mechi za Jumamosi Ligi Kuu England…
Man City 1-1 Liverpool
Burnley 1-2 West Ham
Luton Town 2-1 Crystal Palace
Newcastle 4-1 Chelsea
Nottingham Forest 2-3 Brighton
Sheffield United 1-3 Bournemouth
Brentford 0-1 Arsenal