Liverpool, England
Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp amesema kitendo cha mshambuliaji wake, Mohamed Salah kuweka rekodi mpya ya mabao katika klabu hiyo kwenye Ligi Kuu England ni jambo kubwa la kipekee.
Salah alifunga mabao mawili Jumapili hii katika ushindi mnono wa mabao 7-0 dhidi ya Man United na hivyo kufikisha jumla ya mabo 29 ya ligi na hatimaye kumpiku kinara wa mabao wa zamani wa timu hiyo, Robbie Fowler.
“Hakika hili ni jambo la kipekee, na tusisahau hilo kwa sababu tu tumezowea kumuona akifunga mabao mara nyingi, ni lazima awe mwenye kujivunia kwa hilo,” alisema Klopp kuhusu Salah.
“Matokeo makubwa, kiwango cha juu,” alisema Klopp akizungumzia ushindi huo uliotokana na mabao ya Salah, Cody Gakpo na Darwin Nunez, ambao kila mmoja alifunga mabao mawili na Roberto Firmino aliyefunga bao moja.
Salah ambaye sasa anakuwa ameifunga Man United katika mechi ya sita mfululizo kwenye mashindano yote alisema kwamba tukio hilo ni moja kati ya matukio makubwa katika maisha yake wakati Fowler naye alimpongeza kupitia mtandao wa Twitter.
“Siwezi kulizungumzia hili, ni moja ya siku bora katika maisha yangu, na nimevunja rekodi ambayo nilikuwa nikiiwinda tangu nije katika klabu hii, tuliingia uwanjani kucheza kwa lengo la kushinda,” alisema Salah.
Klopp wakati wote alikuwa mwenye tabasamu huku akiwapungia mkono mashabiki waliofurika kwenye dimba la Anfield na akakiri kwamba kwa namna walivyocheza waliwapa wakati mgumu wapinzani wao.
Ushindi huo unaifanya Liverpool kuibua upya matumaini ya kusaka tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao kwani sasa inashika nafasi ya tano, nyuma ya Tottenham kwa tofauti ya pointi tatu.
Wikiendi ijayo Liverpool itaumana na Bournemouth, timu ambayo mapema msimu huu ilichapwa na Liverpool mabao 9-0. Nini kitaikuta timu hiyo baada ya Man United kuchapwa mabao saba?
