Na mwandishi wetu
Uwanja wa Benjamin Mkapa au Kwa Mkapa kumeendelea kuwa pagumu kwa timu ya Simba baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Azam katika mechi ya Ligi Kuu NBC iliyochezwa Jumanne hii usiku.
Hii inakuwa mechi ya pili mfululizo kwa Simba kutoka katika uwanja huo bila matokeo ya kuridhisha, Jumamosi ilifungwa mabao 3-0 na Raja Casablanca katika Ligi ya Mabingwa Afrika na sasa imebanwa na Azam katika ligi ya NBC.
Aliyeinyima ushindi Simba alikuwa ni Prince Dube, mchezaji nyota wa Azam ambaye nyota yake imeendelea kung’ara katika mechi dhidi ya Simba kwani ndiye aliyefunga bao pekee na la ushindi katika mechi ya mzunguko wa kwanza baina ya timu hizo, mechi ambayo Azam ilishinda kwa bao 1-0.
Safari hii bao la Dube lilikuja mapema mno, takriban katika sekunde 20 baada tu ya mpira kuanza ambapo mfungaji huyo aliitumia vyema pasi ya Akaminko James kuizamisha Simba.
Simba walipambana na kadri muda ulivyokwenda kulikuwa na kila dalili kwamba wangepoteza mchezo huo kabla ya beki wa Azam kujifunga dakika ya 90 wakati akiokoa mpira wa kichwa uliopigwa na Kibu Dennis aliyeingia akitokea benchi.
Mashabiki Azam wanaweza kuyafurahia matokeo hayo lakini kwa kocha wa timu hiyo, Dani Cadena hayajatimiza ahadi aliyoitoa ya kuifunga Simba kama alivyonukuliwa na GreenSports siku chache zilizopita
Kwa matokeo hayo Simba wakiwa wamecheza mechi 23 sasa wanafikisha pointi 54 huku mahasimu wao Yanga ambao Jumatano wikii jioni wataivaa KMC wakiwa na pointi 59 na wameingia dimbani mara 22.
Kwa upande wa Azam wanakuwa katika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 44 baada ya kucheza mechi 23 wakati Singida Big ni wa nne na wana pointi 44 kama Azam na wote wamecheza mechi 23.
Soka Azam yaibana Simba Kwa Mkapa
Azam yaibana Simba Kwa Mkapa
Read also
