Na Hassan Kingu
Safu mpya ya uongozi wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) imepatikana baada ya uchaguzi uliofanyika Jumapili Julai 5, 2026.
Uchaguzi huo hata hivyo umeingia katika sintofahamu baada ya kuibuka habari kwamba washindi halali hawakupewa ushindi badala yake walioshindwa ndio waliopewa ushindi.
Kwa mujibu wa habari hizo nafasi ya urais mshindi aliyetangazwa Leonard Thadeo hakushinda kihalali badala yake mshindi ni Anthony Mtaka ambaye pia ni mkuu wa mkoa wa Njombe na mdau wa mchezo wa riadha.
Matokeo yaliyotangazwa na mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi yalionesha kuwa Thadeo alipata kura 19 kati ya 36 zilizopigwa huku Mtaka akipata kura 11 na mgombea mwingine, Henry Tandau ambaye alikuwa makamu rais wa TOC akiambuia kura sita.
Baadaye zikaja habari zisizo rasmi zikidai kuwa Thadeo ambaye amewahi kuwa mkrugenzi wa idara ya michezo nchini hakushinda kihalali, alipata kura moja na mshindi halali ni Mtaka.
Si sahihi kuamini taarifa zisizo rasmi na ambazo chanzo chake si cha uhakika na cha kuaminika lakini taarifa hizo hizo zisizo rasmi zinaweza kutumika kuutafuta ukweli, kwa maana nyingine huenda kuna ukweli katika taarifa hizo hizo zisizo rasmi.
Sintofahamu katika uchaguzi wa TOC haijaanza kuibuka baada ya matokeo ya uchaguzi bali tangu kuanza kwa mchakato wa uchaguzi wenyewe, dalili za kuchezeana faulo au kukwaza baadhi ya wagombea zilianza kuwa mijadala siku zilizopita.
Matukio hayo ndiyo yaliyosababisha serikali kusimamisha uchaguzi huo na taarifa ya kwanza ya kusimamisha uchaguzi huo ilitangazwa na serikali, Septemba 2025 wakati uchaguzi huo ulipangwa kufanyika Oktoba 4, 2025.
Hoja iliyotolewa na serikali kupitia waziri mwenye dhamana ya michezo wakati huo, Profesa Palamagamba Kabudi ni kwamba TOC katika uchaguzi huo walikuwa wakitumia katiba ya zamani badala ya ile mpya iliyoidhinishwa kisheria na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) mwaka 2020.
Tukio hilo lilipita na mchakato kuanza upya lakini Aprili mwaka huu, uchaguzi huo ukasimamishwa kwa mara ya pili kupitia waziri mwenye dhamana ya michezo, safari hii waziri alikuwa ni Paul Makonda.
Hoja iliyotajwa ya kusimamisha uchaguzi kwa mara ya pili ni mchakato wa uchaguzi huo kutokuwa na uwazi, haki na kukiuka misingi ya utawala bora.
Wakati kauli hiyo ikitolewa wadau wengi walionekana kuunga mkono na hoja kubwa iliyotolewa ni kwamba kuna baadhi ya watu wanaifanya TOC kama mali yao, wanataka kuhodhi madaraka kwa kuwa viongozi wa kudumu na kuwazuia wanaoonekana kutoa ushindani.
Hoja hii ina ukweli hasa kwa kuwa imekuwa kawaida katika chaguzi za TOC kupanga safu za uongozi kwani huko nyuma wagombea wengi waliojaribu kuingia hasa majina mapya na makubwa kwenye michezo waliishia kuaibika au kujitoa kabla hata ya uchaguzi.
Na hili halipo TOC tu, kwenye soka ndio usiseme, upangaji wa safu za uongozi ni jambo la kawaida hivyo wadau au wagombea wanapolalamika kukosekana haki na uwazi unaweza kuona dalili zote za ukweli katika hoja hiyo.
Jambo zuri ni kwamba matukio yote hayo mawili yalipita na uchaguzi ukafanyika kukiwa na amani na matumaini kwa wagombea wakiwamo wale waliolalamikia kukosekana uwazi na haki.
Katika hali ambayo haikutarajiwa, matokeo ya uchaguzi huo yamekuja katika namna ambayo imeibua sintofahamu licha ya uchaguzi wenyewe kufanyika huku kukiwa na matumaini ya uwazi na haki.
Mgombea aliyekuwa akipewa nafasi kubwa na ambaye katika uchaguzi wa awali ilionekana anaogopwa na ndiye anayefanyiwa michezo michafu, hakushinda lakini habari zisizo rasmi zinadai kuwa ndiye aliyeshinda.
Nini kitatokea?
Taarifa za awali kabla ya uchaguzi uliompa ushindi Thadeo kufanyika zilidai kuwa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) imetuma mwakilishi wake katika uchaguzi huo.
Taarifa ya mwakilishi huyo au shuhuda kutoka IOC ndiyo itakayoamua hatma ya Tanzania kimataifa kwenye michezo iliyo chini ya IOC pamoja na ushirikiano wa TOC na IOC ambao unahusisha misaada katika maendeleo ya michezo na mengineyo.
Ni vigumu kwa mtu ambaye hakuwa katika eneo la uchaguzi kujua nini kitatokea lakini waliokuwa kwenye eneo la uchaguzi bila shaka wameshuhudia au kusikia vitendo vya ukiukwaji wa haki kama vilikuwapo katika uchaguzi huo au la.
Mmoja wa mashuhuda hao ni mwakilishi wa IOC, hiyo ndiyo kazi iliyomleta Tanzania na bila shaka ripoti yake ndiyo yenye siri ya Tanzania na hatma ya Tanzania baada ya uchaguzi wa TOC.
Tusubiri lakini tusishangae tukisikia kamati ya mpito imeundwa kwa ajili ya kusimamia shughuli za TOC kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika kwa uhuru na haki na huo kuwa mwisho kwa baadhi ya viongozi waliochaguliwa.
Tusubiri, lakini pia tusishangae siku tutakayosikia viongozi wapya wa TOC wapongezwa na IOC baada ya kushinda katika uchaguzi uliofanyika Julai 5, 2026.
Tusubiri lakini pia tusishangae siku tuyakayosikia Tanzania imeingia katika mkwamo kwa kusimamishwa uanachama IOC na hivyo kutengwa kimataifa katika michezo ikiwamo Michezo ya Olimpiki na viongozi wapya kukosa uhalali.
Kimataifa Nini kitatokea kwa viongozi wapya TOC?
Nini kitatokea kwa viongozi wapya TOC?
Related posts
Read also
