Los Angeles, Marekani
Kocha Mkuu wa Barcelona, Xavi Hernandez ameeleza kushangazwa kwake na timu ya Arsenal kwa jinsi ilivyoonesha ushindani mkubwa na kucheza rafu zenye mbinu hadi kuwafunga mabao 5-3 katika mechi iliyopigwa mjini Los Angeles, Marekani jana Jumatano.
Barca ndiyo iliyoianza mechi hiyo vizuri ikipata mabao mawili yaliyofungwa na Robert Lewandowski na Raphinha kabla Arsenal hawajajibu mapigo kupitia kwa Bukayo Saka, Kai Havertz na Leandro Trossard na hatimaye kuwa mbele kwa mabao 3-2.
Ferran Torres aliisawazishia Barca lakini nyota wa Arsenal, Fabio Vieira aliyeingia akitokea benchi alifunga mabao mawili yaliyotosha kubadili matokeo ya mchezo huo.
“Ilikuwa mechi nzuri kwa mashabiki lakini haikuwa nzuri sana kwa makocha, kulikuwa na kupanda na kushuka, unaweza kusema Arsenal walituzidi na sisi tulikuwa laini kidogo nyuma,” alisema Xavi katika mkutano na waandishi wa habari.
“Ingawa pia kulikuwa na mabaya na mazuri, nilimwambia hata Mikel (Arteta) baada ya mechi kwamba ilikuwa kama mechi ya Ligi ya Mabingwa kwa umakini na ushindani waliouonesha,” alisema Xavi.
“Si jambo la kawaida katika mechi za kirafiki lakini naelewa kwamba kila mmoja alitaka ushindi, kwa upande wetu hiyo ni mechi ya kwanza ya kirafiki,” alisema Xavi.
Kwa upande wake Arteta alikubaliana na Xavi ingawa aliongeza kwamba ushindani haukuwa kwa timu yake tu bali timu zote zilikuwa zikipambana.
Katika dakika 90 za mchezo huo, Arsenal walicheza rafu mara 22 wakati Barca wao walicheza rafu mara 12.