Doha, Qatar
Wenyeji Qatar wamezianza vibaya fainali za Kombe la Dunia baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-0 mbele ya Ecuador katika mechi ya Kundi iliyochezwa leo kwenye Uwanja wa Al Bayt mjini Doha.
Qatar, timu ambayo imekuwa pamoja kwa zaidi ya miezi mitano ikijiandaa na fainali za Kombe la Dunia ilishindwa kuonyesha uwezo wa kukabiliana na Ecuador na sasa ina kazi ngumu ya kukabiliana na wapinzani wengine wa Kundi A, Uholanzi na Senegal, mechi ambazo zitaamua hatma ya timu hiyo kama itasonga mbele au kuishia hatua ya makundi.
Ecuador walionyesha dalili za kupata ushindi mapema baada ya Enner Valencia kuujaza wavuni mpira kwa kichwa lakini mwamuzi alikataa bao hilo kwa msaada wa VAR kwa madai kwamba mfungaji alikuwa ameotea.
Dakika ya 16, juhudi za Ecuador zilizaa matunda kwa bao la penalti lililofungwa na Valencia ambaye aliangushwa na kipa wa Qatar, Saad Al Sheeb ndani ya eneo la penalti na mfungaji kuujaza mpira wavuni kwa shuti la taratibu lililomvuruga Al Sheeb ambaye aliruka upande wake wa kulia na mpira kujaa wavuni upande wa kushoto.
Dakika 15 baadaye, Valencia aliipatia Ecuador bao la ushindi kwa kichwa na kuunyamazisha umati wa mashabiki wa Qatar waliokuwa wakiimba na kuishangilia timu yao kwa muda mrefu kabla ya baadhi ya mashabiki hao kuondoka moja kwa moja uwanjani wakati wa mapumziko.
Qatar haikuonyesha usumbufu wowote kwenye lango la Ecuador japo kuna wakati beki Abdelkarim Hassan alipanda mbele kutafuta bao lakini shuti alilopiga halikuzaa matunda kama ilivyokuwa kwa mshambuliaji mwenye asili ya Tanzania, Akram Afif na mshambuliaji mwenzake Mohammed Muntari wote juhudi zao hazikuweza kubadili matokeo.
Kimataifa Qatar waanza vibaya Kombe la Dunia
Qatar waanza vibaya Kombe la Dunia
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
