Paris, Ufaransa
Wanasoka mastaa, Neymar, Mbappe wa PSG na Cristiano Ronaldo ni miongoni mwa wanasoka wa mwanzo kutuma salamu za rambirambi baada ya kifo cha Pele, mwanasoka anayetajwa kuwa ndiye bora zaidi duniani.
“Mfalme, Pele ndiye aliyebadili kila kitu, kabla ya Pele soka ulikuwa mchezo wa kawaida tu, aliibadili soka na kuwa sanaa, burudani, aliifanya soka kuwa sauti ya watu masikini, watu weusi, aliifanya soka ijulikane Brazil, Soka na Brazil vilipanda hadhi, shukrani kwa mfalme, ameondoka lakini maajabu yake yataendelea kuwapo.” Alisema Neymar.
Kwa upande wake Kylian Mbappe ambaye anacheza timu moja ya PSG na Neymar alisema, “Mfalme wa soka, urithi aliouacha hautosahaulika kamwe.”
Pele ambaye anatajwa kuwa ndiye mchezaji bora katika historia ya soka duniani, alifariki dunia usiku wa Alhamisi kwa maradhi ya saratani akiwa na miaka 82 ameacha rekodi ya kufunga mabao 1,281 katika jumla ya mechi 1,363.
Gwiji huyo ambaye mwaka 2000 alitangazwa na Fifa kuwa mwanasoka bora wa karne, pia ameichezea timu ya Taifa ya Brazil mechi 92 na kuifungia mabao 77 akiwa pia amebeba Kombe la Dunia na timu ya Brazil mwaka 1958, 1962 na 1970, ni mchezaji pekee duniani mwenye rekodi ya kubeba taji hilo kubwa la soka mara tatu.
Naye nyota wa zamani wa Man United na Real Madrid, Cristiano Ronaldo alisema, “kwaheri Mfalme Pele, haitoshi kuelezea maumivu ambayo dunia ya soka inakumbana nayo wakati huu, uungwana ambao Pele aliuonyesha kwangu ulijidhihirisha kwa kila tulichoshirikiana, hata tulipokuwa mbali, kumbukumbu yako itabaki milele kwa kila mmoja wetu anayependa soka.”
Mshambuliaji wa zamani wa Brazil aliyebeba taji la Dunia mwaka 2002, Ronaldo de Lima alimpamba Pele kwa sifa za ubunifu, umahiri, mbinu na umakini usioweza kulinganishwa na kuongeza, “Mfalme wa soka ni Pele mmoja peke yake, shujaa wa wakati wote.”
