London, England
Chelsea jana Ijumaa jioni ilikamilisha usajili wa winga, Noni Madueke (pichani juu) kutoka PSV Eindhoven ya Uholanzi ambaye amesaini mkataba wa miaka saba na nusu.
Madueke, mwenye miaka 20, usajili wake unatajwa kuigharimu Chelsea Dola 38 milioni ambapo katika mkataba wake kuna kipengele kinachompa nafasi ya kuongeza mwaka mmoja.
Makubaliano baina ya Chelsea na PSV yalifikiwa Alhamisi na klabu hiyo kumruhusu mchezaji huyo wa kimataifa wa England kusafiri hadi London kukamilisha taratibu nyingine za usajili.
“Nina furaha kusaini katika moja ya klabu kubwa duniani, kurudi England na kucheza katika Ligi Kuu England ni ndoto kwangu na familia yangu na sina cha kusubiri kabla ya kuanza kucheza England,” alisema Madueke.
“Navutiwa na mambo yajayo ya klabu hii, dira ya mmiliki kwa mambo yajayo na kuwa katika klabu kama hii na hatimaye kushinda mataji ya kiwango cha juu,” alisema Madueke.
Mmiliki na mwenyekiti wa Chelsea, Todd Boehly na wakurugenzi wa bodi walielezea kufurahishwa na usajili wa Madueke hasa kwa kuwa tayari amethibitisha uwezo wake miaka michache iliyopita akiwa PSV akicheza kwenye ligi ngumu na wana furaha kwa uamuzi wake wa kuichagua Chelsea ikiwa ni hatua nyingine katika maisha yake ya soka.
Madueke alijiunga na timu ya vijana ya PSV mwaka 2018 na kucheza kikosi cha wakubwa cha timu hiyo miaka miwili baadaye na hadi sasa ana rekodi ya kuifungia timu hiyo mabao 20 na kutoa asisti 14 katika mechi 80.
Usajili wa Madueke unakua wa sita kwa Chelsea tangu dirisha dogo lifunguliwe Januari mwaka huu, hivi karibuni klabu hiyo iliwasajili Mykhailo Mudryk kutoka Shakhtar Donetsk na Joao Felix kutoka Atletico Madrid.