Na mwandishi wetu
Wakati mjadala mzito wa uhamisho wa kiungo Feisal Salum au Fei Toto kuhamia Azam ukitawala, Yanga imefanikiwa kuwatuliza mashabiki wake baada ya kuichapa Azam mabao 3-2 huku kiungo huyo akikosekana kwenye kikosi cha Yanga.
Ushindi huo uliopatikana Jumapili hii ya Krismasi katika dimba la Benjamin Mkapa, unakuwa tukio kubwa na lenye umuhimu katikati ya mjadala wa Fei Toto ambaye tayari amewaaga mashabiki wa Yanga huku ikidaiwa anaelekea Azam ingawa uongozi wa Yanga haujakubaliana na mpango wa mchezaji huyo kuondoka.
Fei ambaye ilitarajiwa awemo kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga, kukosekana kwake pamoja na Yanga kupata ushindi lakini kunawafanya mashabiki wa timu hiyo waanze kuamini kwamba mchezaji huyo mahiri huenda ni kweli anaondoka.
Nje ya mjadala wa Fei, Azam iliianza vizuri mechi na katika dakika ya 28 iliandika bao la kwanza lililofungwa na Abdul Sopu lakini iliwachukua dakika tatu Yanga kusawazisha mfungaji akiwa ni Fiston Mayele ambaye anaendelea kuwa kinara wa mabao katika Ligi Kuu NBC akiwa sasa amefikisha mabao 14 akimuacha Moses Phiri wa Simba anayeshika nafasi ya pili akiwa na mabao 10.
Dakika mbili baadaye Stephan Aziz Ki akadhihirisha umahiri wake katika mechi kubwa baada ya kuifungia Yanga bao la pili likiwa ni bao jingine muhimu katika Ligi Kuu NBC baada ya lile alilowafunga Simba katika Dar Derby.
Dakika mbili baada ya mapumziko, Sopu aliisawazishia Azam lakini Farid Mussa akaihakikishia Yanga bao la ushindi katika dakika ya 78, bao ambalo lilitokana na juhudi za Aziz Ki aliyeupiga mpira wa adhabu ambao uliokolewa na kipa wa Azam kabla ya kumkuta mfungaji.
Kwa ushindi huo, Yanga imeendelea kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa imefikisha pointi 47 katika mechi 18 ikifuatiwa na Simba yenye pointi 38 katika mechi 17 wakati Azam inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 37 katika mechi 18.
Soka Yanga bila Fei Toto yaipiga Azam
Yanga bila Fei Toto yaipiga Azam
Read also