London, England
Kocha wa England, Gareth Southgate amewajia juu wanaomsakama beki wa timu hiyo, Harry Maguire akisema hajawahi kuona mchezaji akisakamwa namna hiyo ingawa Maguire mwenyewe amesema atakabiliana na jambo hilo.
Maguire (pichani) ambaye pia ni beki wa Man United alijikuta katika wakati mgumu baada ya kujifunga katika mechi ya kirafiki ya England dhidi ya Scotland, mechi ambayo England ilishinda kwa mabao 3-1.
Hiyo ilikuwa mechi ya 59 kwa beki huyo na timu ya England lakini tangu aisaidie timu hiyo kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2018 na kufikia hatua ya nusu fainali na baadaye kuifikisha katika hatua ya fainali ya Euro 2020, amekuwa na wakati mgumu katika klabu na timu ya taifa.
“Sijawahi kuona mchezaji akikumbana na kusakamwa namna hii, amekuwa mchezaji muhimu kwetu na mwenye mafanikio kwa zaidi ya miaka 10, hakika amekuwa tegemeo kwa kipindi hicho, nimekuwa nikizungumzia umuhimu wa wachezaji waandamizi, yeye ni kati yao,” alisema Southgate.
“Wakati wote anapokuwa uwanjani, utulivu ambao amekuwa akiuonesha ni wa kipekee, ni mchezaji wa hadhi ya juu na tuko naye pamoja, mashabiki wetu walikuwa wazuri kwake,” alisema Southgate.
Maguire alivuliwa unahodha katika kikosi cha Man United sababu mojawapo ikiwa ni kukosa namba ya uhakika kikosi cha kwanza lakini pia alihusishwa mno na mipango ya kuuzwa lakini ameendelea kubaki kutokana na janga la mabeki majeruhi katika timu hiyo.
Katika msimu huu wa 2023-24, Maguire amepata nafasi katika kikosi cha Man United, Sepemba 3 akingia kipindi cha pili wakati timu hiyo ikiumana na Arsenal na kulala kwa mabao 3-1.
Katika mechi na Scotland, Maguire alijifunga dakika ya 67 lakini jambo la kushangaza ni kwamba wakati akiingia kutokea benchi katika kipindi cha pili alijikuta akizomewa na mashabiki wa England jambo ambalo lilimkera Southgate.
“Kama ni mashabiki wa Scotland naweza kuelewa na wala sina cha kulalamika kwa walichokifanya lakini hayo ni matokeo ya kusakamwa kwa mchezaji huyo kwa kipindi kirefu,” alisema Southgate.
“Ni dhihaka, si mashabiki wa Scotland tu lakini hata waandishi wetu, wachambuzi wa soka au wowote wale, wametengeneza kitu ambacho sijawahi kukiona hapo kabla,” alisema Southgate.
Kwa upande wake Maguire alisema kwamba walichofanya mashabiki wa Scotland ni kama vile kuwaondolea presha wachezaji wenzake wa England na kuzielekeza kwake jambo ambalo amesema kwamba ni dogo na atakabiliana nalo.