Na mwandishi wetu
Kocha wa timu ya mpira wa kikapu ya Pazi, Mohamed Mbwana amesema kutolewa mapema kwenye mashindano ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika (BAL), kumetokana na wachezaji wake kutokuwa na uzoefu wa kutosha.
Akizungumza baada ya mchezo wa mwisho dhidi ya Dynamo ya Burundi ambayo walipoteza kwa pointi 85-88, Mbwana alisema kingine kilichochangia watoke mapema ni kukosa bahati kutokana na kiwango ambacho kilioneshwa na wachezaji wake.
“Tumekubali matokeo lakini ushiriki wetu umekuwa na faida tumejifunza kitu, kikubwa hapa ni uzoefu mdogo ambao wachezaji wangu wanao lakini nawapongeza walicheza kwa kujituma katika mechi zote nadhani tulikosa bahati,” alisema Mbwana.
Kocha huyo alisema wanarudi kujipanga upya kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye mashindano ya ndani na kucheza mechi kadhaa za kirafiki za kimataifa ambazo anaamini zitasaidia kuwapa wachezaji wake uzoefu kwa ajili ya kufanya vizuri kwenye mashindano yajayo ya Afrika.
Pia kocha huyo aliwaomba radhi mashabiki wao kwa matokeo hayo ambayo wameyapata kwenye mashindano hayo na kueleza kusudio lao ilikuwa ni kufanya vizuri na kurudi na ubingwa ingawa imekuwa tofauti.
Timu zilizofuzu hatua ya nusu fainali kutoka kundi A ilipokuwa Pazi ni Dynamo ya Burundi na Capetown Tigers ya Afrika Kusini.
Katika mashindano hayo Pazi ilipoteza mechi zote tatu za hatua ya makundi, mbali ya Dynamo pia ilipoteza dhidi ya NBA Academy kwa pointi 57-84, ikafungwa na Capetown Tigers kwa pointi 87-95.
