Barcelona, Hispania
Klabu ya Barcelona imemuomba radhi mshambuliaji wa Real Madrid, Vinícius Junior baada ya mmoja wa wakurugenzi wake kupuuza dhihaka za kibaguzi dhidi ya mshambulaiji huyo akisema kwamba anahitaji ‘kupigwa kofi’
Mkurugenzi huyo, Miquel Camps ambaye pia ni mjumbe wa bodi ya klabu hiyo alitoa kauli hiyo kupitia mtandao wa Twitter sasa X wakati wa mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya Real Madrid na Braga Jumanne usiku.
Mara baada ya kutoa kauli hiyo, Camps kwa haraka ilifuta andiko lake ingawa tayari lilishaanza kuwa mjadala miongoni mwa watumiaji wa mtandao huo hasa nchini Hispania.
“Si tu ubaguzi wa rangi bali alitakiwa kupigwa kwa kuwa mtu wa vituko, yale mambo yasiyo na maana uwanjani alikuwa anafanya kwa nini,” alisema Camps kupitia mtandao wa X.
Mara baada ya Barca kucheza mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Shakhtar Donetsk Jumatano usiku, makamu rais wa klabu hiyo, Rafa Yuste alisema kwamba andiko hilo halina nafasi na haliwezi kurudiwa tena.
“Kama Vinícius atataka kunisikiliza mimi, nataka kumwambia kwamba hili jambo halitatokea tena, hata kama ni kosa lakini hlikutakiwa kuwekwa kwenye mitandao, halikuwa andiko sahihi,” alisema Yuste.
Vinícius ambaye pia ni mshambuliaji wa timu ya taifa ya Brazil, amejikuta akiandamwa na dhihaka za kibaguzi kutoka kwa mashabiki katika mechi za La Liga ikiwamo mechi ya mwishoni mwa wiki iliyopita dhidi ya Sevilla.
Mashabiki na wadau wengi wa soka wanasubiri kuona kama Vinicius atakutana na hali hiyo Jumamosi ijayo wakati wa mpambano wa El Clásico unaowahusisha vigogo wa soka la Hispania, Real Madrid na Barca.
