Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amesema pamoja na ushindi mnono walioupata katika mechi za hivi karibuni lakini bado timu yake haijaonesha kiwango kile ambacho anatamani kukiona.
Katika mechi tatu zilizopita ikiwemo moja ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga wamefunga jumla ya mabao 15 na kuruhusu bao moja la mkwaju wa penalti dhidi ya Asas ya Djibout, huku waking’ara katika kuutawala mchezo kwa asilimia kubwa ya mechi hizo.
Akizungumza katika mahojiano na Azam Media, kocha huyo raia wa Argentina alisema timu yake bado inakosa muunganiko mzuri ambao kwa sasa ndio kitu anachokifanyia kazi kwenye uwanja wa mazoezi na endapo hilo litatimia, anaamini watakuwa bora kuliko wanavyoonekana hivi sasa.
“Nafurahi kuona tunapata ushindi wa mabao mengi na mashabiki wetu wanafurahi lakini bado timu haichezi kwa ubora ninaoutaka, tunakosa muunganiko mzuri kwa baadhi ya wachezaji kama Hafiz Konkoni, Mahtlas Makudubela, Gift Fred na wengineo ambao pia naridhishwa na mwenendo wao, siku tukikamilisha muunganiko tutakuwa moto zaidi ya ilivyo sasa,” alisema Gamondi.
Kocha huyo alisema anajiona mwenye bahati kuifundisha timu yenye wachezaji wenye uwezo na vipaji vikubwa vya kucheza mpira kwani hilo linafanya kazi yake kuwa rahisi zaidi kuliko alivyotarajia wakati akisaini mkataba wa kuifundisha timu hiyo.
Alisema kwa muda mfupi alioifundisha Yanga amejua mambo mengi kuhusu timu hiyo ikiwemo namna mashabiki wanavyoipenda timu yao na kujua mambo mengi yanayowahusu wachezaji, hilo kwake ni jambo zuri kwani linamfanya hata yeye na wenzake wa benchi la ufundi kuwa makini.
Katika michezo saba ambayo amekiongoza kikosi cha Yanga, Gamondi amepoteza mchezo mmoja wa fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba na kushinda mechi sita dhidi ya Kaizer Cheifs, Asas Telcom mechi mbili, Azam FC, KMC na JKT Tanzania.