Na mwandishi wetu
Bondia Mtanzania, Hassan Mwakinyo amethibitisha rasmi uwepo wa pambano la marudiano baina yake na Liam Smith linalotarajiwa kufanyika Januari 23, mwakani.
Imeelezwa kwamba hatua ya kuhitajika wawili hao kurudiana imekuja baada ya promota wa pambano hilo, Benjamin Shalom kutoridhishwa na maamuzi ya mwamuzi wa pambano la awali lililopigwa Jumamosi iliyopita na Mwakinyo kupoteza kwa TKO.
Mwakinyo alipoteza kwa TKO raundi ya nne ya ‘ringi’ hiyo iliyokuwa na raundi 12 iliyopigwa jijini Liverpool, England dhidi ya Muingereza huyo baada ya kujiumiza kifundo cha mguu na kuanguka.
Ingawa aliendelea na pambano lakini alipiga goti mara mbili huku akijitahidi kuonyesha ishara ya kutaka kusimamishwa pambano kwanza akionekana kuugulia maumivu lakini mwamuzi aliamua kumaliza pambano.
“Kutokana na mchezo uliopita na kitendo cha refa kuwa ‘unfair’ kwangu kimemlazimu promota Benjamin Shalom kutupa nafasi ya kurudiana na Liam Januari 23. Nina nguvu ya kutosha kwa ajili ya mechi ya marudiano,” ameandika juzi Mwakinyo kupitia ukurasa wake mtandao wa Instagram.
Mwakinyo amepoteza pambano hilo akiwa amerudi ulingoni baada ya kupita zaidi ya miezi 10 tangu alipopigana mara ya mwisho na Julius Indongo mwezi Septemba, mwaka jana.
Kulingana na Mwakinyo kuanza vizuri pambano lake dhidi ya Liam imepelekea wadau wengi kutaka kuona marudiano yao ikizingatiwa namna mechi hiyo ilivyomalizika kwa utata, Mwakinyo akidai alipewa viatu ambavyo vilimbana na kumuumiza kifundo cha mguu.
Ngumi Mwakinyo, Liam kurudiana Januari
Mwakinyo, Liam kurudiana Januari
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
