Na mwandishi wetu
Kipa wa Simba, Ally Salim leo Alhamisi amefanikiwa kushinda tuzo ya mchezaji bora wa mashabiki wa Simba mwezi Aprili akiwazidi kiungo mshambuliaji, Kibu Denis na mshambuliaji Jean Baleke.
Ally ambaye kwa mara ya kwanza amepewa nafasi kwenye mechi tano mfululizo za Wekundu hao baada ya kuelezwa kuumia kwa Aishi Manula, amechukua tuzo hiyo kutokana na uwezo mkubwa aliouonesha kwenye mechi nne za mwezi Aprili.
Katika mwezi huo, Salim alifanikiwa kumaliza mechi tatu bila ya kuruhusu bao ambapo walishinda mabao 2-0 dhidi ya Ihefu na kupata ushindi kama huo tena dhidi ya Yanga kabla ya kuifunga Wydad CA ya Morocco bao 1-0.
Salim aliruhusu bao kwenye mechi ya marudiano dhidi ya Wydad kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya robo fainali.
Kwenye mechi hizo, Kibu alifunga bao moja na Baleke raia wa DR Congo anayeichezea Simba kwa mkopo akitokea TP Mazembe, alifunga mabao matatu.
Salim ambaye anakuwa kipa wa kwanza kushinda tuzo hiyo iliyoanzishwa miaka miwili iliyopita atakabidhiwa pesa taslimu Sh. 2,000,000 na tuzo kutoka kwa wadhamini wa tuzo hiyo Emirate Aluminium Profile.
Soka Ally Salim atwaa tuzo Simba
Ally Salim atwaa tuzo Simba
Read also