Miami, Maarekani
Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Argentina, Lionel Messi amesema alichukizwa kwa kutopewa heshima na klabu yake ya zamani wa PSG baada ya kubeba kombe la dunia wakati wachezaji wenzake wote wa Argentina walipewa heshima hiyo na klabu zao.
Katika mechi ya fainali kati ya Argentina na Ufaransa, Messi alifunga mabao mawili na lingine la tatu kwenye mikwaju ya penalti na kuiwezesha Argentina kutoka na ushindi wa 4-2 na hatimaye kubeba Kombe la Dunia katika fainali zilizopigwa Qatar, Novemba na Desemba mwaka jana.
Akizungumzia hali ilivyokuwa baada ya ushindi huo aliporejea katika klabu yake Messi alisema, “mimi nilikuwa mchezaji pekee kati ya 25 ambaye sikupewa heshima na klabu.”
Messi katika hilo alifafanua, “inaeleweka, kwa sababu sisi (Argentina) wao (Ufaransa) hawakuweza kulitetea Kombe la Dunia.”
Katika usajili wa dirisha kubwa la kiangazi, mwezi Juni, Messi aliachana na PSG na alikuwa na wakati mgumu katika klabu hiyo na alikiri kwamba kulikuwa na tatizo kati yake na baadhi ya mashabiki wa klabu hiyo katika misimu miwili aliyoichezea.
Alipoulizwa kama hakupenda kujiunga na PSG, Messi alisema, “Ilitokea kama ilivyokuwa, halikuwa jambo ambalo nililitarajia lakini wakati wote huwa nasema, kuna mambo hutokea kwa sababu, hata kama sikuwa vizuri pale lakini ilitokea kwamba nilikuwa bingwa wa dunia wakati nikiwa pale.”
Akiizungumzia klabu yake ya sasa ya Inter Miami FC ya Marekeni, Messi alisema kwamba anafurahia soka lake katika klabu hiyo.
“Napenda ninachokifanya, nafurahia kucheza na kwa sasa nacheza katika namna tofauti, na hii ndio sababu iliyonifanya nichukua uamuzi wa kuja Miami na si kuendelea na soka kwingineko, unapata uzoefu tofauti,” alisema Messi.
Kuhusu uwezekano wa kustaafu soka, Messi mwenye umri wa miaka 36 sasa alisema kwamba hafikirii jambo hilo na hajaufuta uwezekano wa kurudi nyumbani Argentina na kuichezea klabu yake ya zamani ya utotoni ya Newell’s Old Boys kabla ya kustaafu soka hasa baada ya kuwa tayari amebeba taji la dunia.