Na mwandishi wetu
Jumamosi imekuwa siku ya hovyo kwa timu ya Simba baada ya kukubali kichapo cha mabao 3-0 mbele ya Raja Casablanca kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Matokeo hayo yanatibua rekodi nzuri ya Simba katika mechi za makundi za CAF kwenye uwanja huo, rekodi ambayo imekuwa ikiambatana na usemi maarufu wa kwa Kwa Mkapa hatoki mtu.
Hata hivyo Jumamosi ya Februari 18, 2023, ametoka mtu Kwa Mkapa, tena ametoka kwa ushindi wa kishindo, ‘mtu huyo’ ni Raja Casablanca, timu kutoka nchini Morocco.
Mambo yalianza kuwaharibikia Simba katika dakika ya 30 baada ya Hamza Khaba kuandika bao la kwanza kwa shuti la nje kidogo ya 18 akiitumia pasi ya Zakaria Habti.
Simba wakiitambua ahadi ya Sh 5 milioni ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kila bao, walipambana na kulisakama lango la Raja, mfano dakika ya 35, Pape Sakho alishindwa kuitumia vizuri pasi aliyopewa na Saido Ntibazonkiza kuipatia Simba bao. Sakho baadaye alitolewa na kuingia Moses Phiri.
Ntibazonkiza ambaye amerejea kwa mara nyingine kwenye kikosi cha Simba baada ya kukosekana mechi iliyopita, alionyesha uhai na kuongoza vyema mashambulizi pamoja na Clatous Chama lakini hadi mapumziko, wageni Raja walikuwa mbele kwa bao hilo.
Kipindi cha pili kasi ya Simba iliongezeka na mara kadhaa walilifikia lango la Raja ambao kwa muda wa takriban dakika 20 kazi yao kubwa ilikuwa kuokoa na kuvuruga mipango ya Simba.
Mabadiliko yaliyofanywa na kocha Roberto Olivieira a’ Robertinho ya kuwatoa John Bocco na nafasi yake kuingia Jean Baleke na Ismail Sawadogo na nafasi yake kuingia John Mkude yalizidi kuipa nguvu Simba lakini nafasi kadhaa ilizotengeneza timu hiyo hazikuzaa matunda.
Bocco kabla ya kutoka alipata nafasi nzuri lakini akajichanganya wakati wa kupiga mpira na Baleke naye muda mfupi baada ya kuingia aliunganishiwa pande na Chama lakini akashindwa kuipa Simba bao.
Simba ilikatishwa tamaa dakika ya 83 iliporuhusu bao la pili lililofungwa na Soufian Benjdida kabla ya kuruhusu la tatu dakika tatu baadaye lililofungwa kwa penalti na Mokaden. Penalti hiyo ilitokana na rafu ya Joash Onyango katika eneo la penalti.
Baada ya matokeo hayo, kocha Robertinho alisema kwamba kazi bado inaendelea kwa mechi zilizobaki ambazo wanaweza kuzitumia kuipatia Simba mafanikio.
Kwa Raja huo ni ushindi wa pili mkubwa baada ya ushindi wa mabao 5-0 katika mechi ya kwanza dhidi ya Vipers ya Uganda wakati Simba inakuwa imepoteza mchezo wa pili baada ya kulala kwa bao 1-0 katika mechi ya kwanza dhidi ya Horoya ya Guinea.
Kikosi cha Simba kilichoanza: Manula, Kapombe, Zimbwe Jr, Onyango, Inonga, Sawadogo, Ntibazonkiza, Mzamiru, Bocco, Chama na Phiri.
Kimataifa Raja yaivuruga Simba kwa Mkapa
Raja yaivuruga Simba kwa Mkapa
Read also
