Na mwandishi wetu
Juni 5 ya kila mwaka ni Siku ya Mazingira Duniani, makundi ya wanamazingira huitumia siku hiyo kuihamasisha jamii umuhimu wa kuyajali, kuyatunza na kuyalinda mazingira.
Juni 5 imekuwa ikifanywa Siku ya Mazingira Duniani tangu miaka 50 iliyopita, sherehe zimekuwa zikifanyika huku kukiwa na kauli mbiu tofauti zinazoandamana na tukio zima la Siku ya Mazingira.
Kwa mwaka huu mwenyeji wa Siku ya Mazingira Duniani ni nchi ya Ivory Coast ambapo kauli mbiu ya siku hiyo inahusu suluhisho la uchafu utokanao na plastiki.
Wakati makundi mbalimbali yakijitahidi kuienzi na kuipa thamani Siku ya Mazingira Duniani, kwa wanamichezo hasa wa Tanzania bado mwamko umekuwa mdogo katika kuipa hadhi siku hiyo.
Kwa mfano licha ya kuwapo umuhimu mkubwa wa kuyatunza mazingira kwa ustawi wa michezo, ni wanamichezo wachache mno nchini kama wapo wanaojua kwamba jana Jumatatu Juni 5, ilikuwa Siku ya Mazingira Duniani.
GreenSports tunaamini nguvu ya wanamichezo inahitajika katika kuitumia siku hii kuihamasisha jamii umuhimu wa kuyatunza na kuyalinda mazingira ili kukabiliana na matatizo mbalimbali yanayotokana na uharibifu wa mazingira yakiwamo Mabadiliko ya Tabianchi.
Suluhisho la matatizo mengi yanayotokana na ubaribifu wa mazingira ni upandaji miti, GreenSports tunadhani hili ni eneo ambalo wanamichezo wanatakiwa kusimama kidete katika kuunga mkono kampeni ya upandaji miti inayoongozwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).
Wanamazingira mara kadhaa wamekuwa wakizitaja faida za misitu, mojawapo ni ukweli kwamba miti ni chanzo cha hewa safi hivyo wanamichezo lazima watambue kwamba upandaji miti ni jambo lenye faida kwao na wana wajibu wa kuunga mkono kampeni ya upandaji miti kwani raha ya michezo ni pamoja na uwapo wa hewa safi.
Katika hili wanamichezo waige mfano wa mwanariadha wa Kenya, Eliud Kipchoge ambaye ni bingwa mara mbili wa mbio za Olimpiki, amewahi kusema kwamba majanga ya uharibifu wa mazingira yanaweza kumfanya ahindwe kufurahia mchezo wa riadha anaoupenda.
Mwanariadha huyu anaamini kwamba hewa safi ni kitu muhimu katika kumfanya akimbie vizuri na kuufurahia mchezo wa riadha.
Kwa sasa Kipchoge (pichani juu) anaendesha kampeni za upandaji miti nchini Kenya akishirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Kenya (KFS) akiamini kwamba kuna uhusiano mkubwa kati ya hewa safi, mchezo wa riadha na michezo mingine.
Nchini Sweden katika hafla ya Siku ya Mazingira Duniani mwaka 2022, nchi hiyo iliwatumia vizuri wanamichezo katika kuipa thamani na hadhi siku hiyo na kuihamasisha jamii kutunza mazingira.
Katika hilo watoto zaidi ya 6,000 walishiriki katika mbio fupi katika Jiji la Stockholm ili kuonyesha uhusiano uliopo kwenye michezo na umuhimu wa hewa safi kwa wanamichezo wa sasa na baadaye.
Kwa mantiki hiyo, GreenSports tunaamini huu ni wakati sahihi kwa wanamichezo wetu si tu kujua uwapo wa Siku ya Mazingira Duniani bali pia kuienzi siku hiyo na kuipa thamani yake kwa ustawi wa jamii na maendeleo ya michezo.
GreenSports Wanamichezo waienzi Siku ya Mazingira
Wanamichezo waienzi Siku ya Mazingira
Read also
