Na mwandishi wetu
Wakati Yanga na Azam zikijiandaa kuumana keshokutwa Jumapili, kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi amekiri kuutambua ubora wa Azam lakini wataingia kwenye mchezo huo wakiwa na lengo la kutafuta pointi tatu zitakazowafanya waendelee kuongoza mbio za kutwaa taji la Ligi Kuu NBC.
Yanga ambao watakuwa ugenini kwenye mchezo huo wataingia wakiwa na kumbukumbu ya kuondoka na pointi moja kwenye mechi ya mzunguko wa kwanza walipolazimishwa sare ya mabao 2-2 kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu NBC watashuka kumenyana na Azam wakiwa kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa na pointi 44 ikifuatiwa na Simba wenye alama 38 na Azam wenye pointi 37.
“Hii ni mechi muhimu kwa kila timu kwa sababu kila mmoja wetu anahitaji pointi, kwa upande wetu tuko makini na maandalizi yetu, pia kufanyia kazi madhaifu ya kikosi chetu, pamoja na kuhakikisha tunatumia vema nafasi tunazopata hasa kipindi cha kwanza cha mchezo.
“Tunatambua ubora na uimara wa Azam kwa kuangalia baadhi ya mechi zao, walizocheza siku za karibuni ili angalau tuingie kwa mbinu tofauti na michezo iliyopita ya ligi,” alisema Nabi raia wa Tunisia.
Naye Kocha wa Azam, Kali Ongala alisema baada ya mchezo wao wa mwisho dhidi ya Geita Gold, walienda kuweka kambi ya siku tatu jijini Mwanza na wamerejea leo asubuhi wakiwa tayari kwa ajili ya kuwavaa wapinzani wao hao.
“Maandalizi yetu yako vizuri na tuko tayari kwa mchezo wetu huo, utakuwa wa ushindani mkubwa kwa sababu kila mmoja wetu anahitaji kufikia malengo, tunawaheshimu Yanga na tutaonyesha mchezo mzuri dhidi yao.
“Tumetoka kupata sare mbili mfululizo ugenini, tunarudi nyumbani kuzisaka pointi tatu ambazo zitainua ari yetu ya kushinda kama tulivyofanya michezo iliyopita, naamini hili litafanikiwa iwapo tutarekebisha makosa ya kwenye mechi zetu zilizopita,” alisema Ongala.
