Na mwandishi wetu
Mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Fiston Mayele amesema kuwa iwapo kiungo Stephan Aziz Ki ataendelea kuwa na ubora alionao sasa atanyakua kiatu cha ufungaji bora Ligi Kuu NBC msimu huu.
Mayele alisema hayo baada ya Aziz Ki kufikisha mabao 10 kwenye orodha ya wafungaji wa ligi kuu akiwa ameshuka uwanjani mara 11 akiwa na wastani wa kufunga bao moja kwenye kila mchezo.
Mayele aliyekuwa Yanga msimu uliopita na sasa akikipiga Pyramids ya Misri, msimu uliopita alinyakua kiatu hicho baada ya kupachika mabao 17 akiwa sawa na Saido Ntibazonkiza wa Simba.
Mshambuliaji huyo raia wa DR Congo alisema hashtushwi na kinachofanywa na Aziz Ki kutokana na ubora alionao na wala hatashangaa akimuona akishinda tuzo ya mfungaji bora.
“Nimekuwa nikimuangalia nini anafanya, amekuwa na muendelezo mzuri tangu msimu ulipoanza kama ataendelea hivi basi kiatu cha ufungaji ataenda kukitwaa,” alisema Mayele.
Mayele alisema kuwa kinachombeba Aziz Ki ni hamu aliyonayo ya kufanya mambo makubwa kwa ajili ya timu pamoja na kujituma kwenye uwanja wa mazoezi.