London, England
Kocha wa England, Gareth Southgate ataendelea kukinoa kikosi cha timu hiyo hadi baada ya fainali za Ulaya 2024 (Euro 2024). Chama cha Soka England (FA) kimethibitisha hilo.
Mara baada ya England kutolewa kwenye fainali za Kombe la Dunia katika hatua ya robo fainali, Southgate alisema kwamba angekaa na mabosi wa FA kwa lengo la kujadiliana kuhusu hatma yake ndani ya kikosi hicho.
Kocha huyo mweny umri wa miaka 52 alipewa majukumu ya kuinoa timu hiyo mara ya kwanza mwaka 2016 akichukua mikoba ya Sam Allardycee na kuiongoza hadi hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2018 pamoja na kuifikisha kwenye hatua ya fainali katika Euro 2020.
“Kwa furaha kubwa tunathibitisha kwamba Gareth Southgate ataendelea kuwa kocha wa England na atatuongoza katika kampeni zetu za Euro 2024,” ilieleza taarifa ya FA iliyosainiwa na mtendaji mkuu Mark Bullingham kuhusu kocha huyo ambaye mkataba wake unafikia ukomo Desemba 2024.
“Gareth na Steve Holland (kocha msaidizi) wakati wote tumekuwa tukiwaunga mkono na mipango yetu ya Euro 2024 ndio inaanza sasa. Southgate kwa sasa ni lazima awe mshindi ambaye England inamtaka,” ilifafanua taarifa hiyo ya Bullingham.
Southgate mwanasoka na beki wa zamani, anasifika kwa kuimarisha mshikamano na umoja katika kikosi cha England hata baada ya timu hiyo kutolewa kwenye fainali za Kombe la Dunia amekuwa akipigiwa debe aendelee kuinoa timu hiyo akiwa hadi sasa ameshinda jumla ya mechi 49 kati ya 81 na kupoteza 14 ingawa bado hajaweza kuipa taji timu hiyo.
Southgate kwa sasa anashika nafasi ya nne kwa kuiongoza timu ya England katika mechi nyingi akiwa ametanguliwa na Walter Winterbottom (mechi 139), Sir Alf Ramsey (mechi 113) na Sir Bobby Robson (mechi 95).
Kimataifa Southgate kuendelea kuinoa England
Southgate kuendelea kuinoa England
Read also