Manchester, England
Klabu ya Manchester United imesema bado haijaamua lolote kuhusu kumrudisha kikosini mchezaji wake Mason Greenwood na kwamba jambo hilo linahitaji tafakuri ya kina kabla ya kufikia uamuzi.
Msimamo huo unazidi kumuweka njia panda mshambuliaji huyo ambaye Februari mwaka huu alifutiwa mashtaka yaliyokuwa yakimkabili akituhumiwa kutaka kubaka pamoja na udhalilishaji wa kijinsia.
Awali Man United walitarajia kutoa uamuzi kuhusu Greenwood kabla ya Jumatatu iliyopita, siku ambayo timu hiyo ilicheza mechi ya kwanza ya Ligi Kuu England (EPL) msimu wa 2023-24 dhidi ya Wolves.
Jana Jumatano taarifa ya klabu hiyo ilieleza kuwa uchunguzi wa kutafuta ukweli kuhusu Greenwood tayari umekamilika na uamuzi wa mwisho upo mikononi mwa ofisa mtendaji mkuu Richard Arnold ambaye yuko katika hatua za mwisho.
Klabu ya Man United imekuwa ikiangalia zaidi suala la Greenwood kurudi katika kiwango kilicho bora lakini uzito wa mjadala unaoendelea kuhusu mchezaji huyo umeifanya klabu hiyo itulie na kuendelea kulifanyia tafakuri zaidi kabla ya kuamua kumrudisha kikosini au la.
Katika kulifanyia kazi sakata la mchezaji huyo, Man United imekusanya taarifa ambazo hazijulikani na wengi kutoka kwa watu waliohusika moja kwa moja au wenye uelewa wa jinsi tukio zima lilivyokuwa.
“Pia tuna jukumu kwa Mason kama waajiriwa wake, kama kijana mdogo ambaye amekuwa na klabu hii tangu akiwa na umri wa miaka saba,” ilieleza taarifa ya Man United.
“Tofauti na uvumi wa kwenye vyombo vya habari, hakuna uamuzi wowote uliofikiwa na sasa suala hilo lipo katika uchunguzi wa kina, uamuzi utakapofikiwa tutatangaza na kutoa ufafanuzi kwa wahusika wa ndani ya klabu na wadau wengine,” ilifafanua taarifa hiyo.
Miongoni mwa wadau ambao inadaiwa watahusika katika mashauriano kabla ya kufanya uamuzi wowote ni pamoja na mabosi wa timu ya wanawake ya Man United.
Kimataifa Greenwood njia panda Man United
Greenwood njia panda Man United
Read also