Na mwandishi wetu
Kipa mpya wa Yanga, Metacha Mnata amesema kuwa ametua timu hiyo ili kuleta ushindani wa kugombania namba katika kikosi cha kwanza cha vinara hao wa Ligi Kuu NBC.
Metacha ametua Yanga hivi karibuni katika usajili wa dirisha dogo kwa ajili ya kuongeza nguvu baada ya kuumia kwa kipa namba mbili Aboutwalib Mshery.
Kipa huyo alikiri kuwa kipa namba moja wa Yanga, Djigui Diarra anafanya vizuri kwa sasa lakini atajitahidi kuonesha uwezo kwenye mazoezi ili kumshawishi kocha ampe nafasi ya kucheza.
“Nimekuja hapa kumsaidia Diarra katika kupigania mafanikio ya Yanga, najua si kazi rahisi kumtoa kwenye nafasi hiyo kutokana na ubora wake na kiwango anachokionesha kwa sasa lakini nitapambana ili kumshawishi kocha anipe nafasi ya kucheza,” alisema Metacha.
Alisema mbali na kuwa tayari kupigania namba lakini kufanya kazi na kipa huyo raia wa Mali anaamini kutamsaidia kujifunza mambo mengi kutokana na uzoefu aliokuwa nao kwa kushiriki mashindano makubwa Afrika.
Yanga imemsajili Metacha kwa mkopo wa miezi sita na hiyo ni baada ya kuvutiwa na kiwango chake akiwa na timu yake ya Singid Big Stars msimu huu.
