Na mwandishi wetu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa amejipanga kuziimarisha sekta za utamaduni, sanaa na michezo ili kuhakikisha matarajio ya serikali na wananchi yanafikiwa.
Msigwa aliyasema hayo jana jijini Dodoma wakati akikabidhiwa ofisi na Balozi Saidi Yakubu ambapo ametaja kipaumbele chake cha kwanza kuw ni kuhakikisha anaziongezea sekta hizo kasi, ubunifu na kuleta matokeo chanya.
“Watanzania wanahitaji furaha na hii ndio wizara ambayo inasimamia utekelezaji wa sera zinazowawezesha kupata furaha, hivyo nimejiandaa kuhakikisha maeneo yote katika sekta hizi tatu yanakwenda kwa kasi zaidi, nguvu, ari na ubunifu mkubwa”, alisema Msigwa.
Kuhusu michezo, Msigwa alisema kwa sasa kuna majukumu mazito ikiwemo maandalizi ya michuano ya Mataifa ya Afrika 2027 (Afcon) ambapo Tanzania, Kenya na Uganda ni waandaji wa mashindano hayo.
Kwa kutazama zaidi miundombinu iliyopo kwenye utamaduni, Msigwa alisema Tanzania ina mengi yanayohusu sekta ya utamaduni ambapo mtazamo wake ni kujenga taasisi imara zinazosimamia utamaduni kama ambavyo imefanyika kwa kiasi kwenye sanaa na michezo.