Riyadh, Saudi Arabia
Straika wa Real Madrid, Karim Benzema inadaiwa anafikiria upya uamuzi wa kuendelea kuichezea timu hiyo baada ya kutangaziwa Pauni 346 milioni na mkataba wa miaka miwili nchini Saudi Arabia.
Benzema mwenye umri wa miaka 35 ambaye pia mwaka jana alitwaa tuzo ya Ballon d’Or, inadaiwa alishafanya mazunguimzo ya awali ya kuongeza mkataba Real Madrid lakini donge nono la Saudi Arabia limemlazimisha kufikiria upya.
Straika huyo ambaye msimu uliopita aliiwezesha Real Madrid kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, msimu huu hadi sasa ameifungia timu hiyo mabao 30 katika mechi 42 na bado anahitajika kwa ajili ya msimu ujao.
Habari zaidi zinadai kwamba straika huyo Mfaransa kama mambo yake yatakwenda vizuri nchini Saudi Arabia atakuwa na maslahi yanayolingana na ya Cristiano Ronaldo ambaye aliondoka Man United na kujiunga na klabu ya Al Nassr ya mjini Riyadh.
Mapema mwezi huu, Benzema inadaiwa aliwahakikishia mabosi wa Real Madrid kwamba yuko tayari kuongeza mwaka mwingine mmoja na klabu hiyo lakini katika wiki za karibuni ameonekana kubadili mawazo baada ya ofa ya Saudi Arabia.
Msimu huu haukuwa mzuri kwa Benzema, hali ilianza kuwa mbaya wakati wa fainali za Kombe la Dunia Desemba mwaka jana, aliondolewa katika kikosi cha Ufaransa kutokana na kuwa majeruhi.
Kwa upande wa Real Madrid, timu hiyo imeshindwa kulibeba taji la Ligi Kuu Hispania yaani La Liga lakini pia imeishia hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kutolewa na Man City.
Azma ya mchezaji huyo ilikuwa wazi mapema kwamba msimu ujao angeendelea kuvaa jezi ya Real Madrid, timu aliyoichezea kwa miaka 11 sasa lakini amebadili mawazo na haitoshangaza akimfuata Ronaldo, mchezaji mwenzake wa zamani wa Real Madrid nchini Saudi Arabia.
Mchezaji mwingine anayehusishwa na mipango ya kwenda kucheza soka Saudi Arabia ni Lionel Messi ambaye kama ilivyo kwa Benzema haijajulikana atajiunga na timu gani ingawa zinazotajwa zaidi ni Al Nassr na Al Hilal ambazo ni timu mahasimu katika jiji la Riyadh.
Messi ambaye amemaliza mkataba na PSG ya Ufaransa msimu huu, pia anahusishwa kwa nguvu na mipango ya kurudi klabu yake ya zamani ya Barcelona.
Kimataifa Ofa ya Saudi Arabia yamfikirisha Benzema
Ofa ya Saudi Arabia yamfikirisha Benzema
Read also