Na mwandishi wetu
Uongozi wa timu ya Singida Big Stars umekanusha taarifa zinazoenea kuwa wako kwenye mikakati ya kubadilishana kiungo wao Mbrazili Dario Junior na Jesus Moloko wa Yanga.
Fununu hizo zilienea tangu jana ikielezwa kuwa Yanga wamevutiwa na kiwango cha mchezaji huyo katika mechi mbili za kirafiki alizocheza dhidi ya Zanaco ya Zambia na Mtibwa Sugar na hivyo kuanza ushawishi wa kumnasa mchezaji huyo kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili.
Mtendaji Mkuu wa Singida, Dismas Ten amefafanua kuwa japo wanafahamu soka ni biashara lakini kwa sasa hawako tayari kufanya hivyo na hakuna ukweli wowote kuhusiana na hilo.
“Hizi taarifa hazikutoka Singida Big Stars, kwa hiyo huko zilikotoka tunaziacha ziendelee kutoka lakini rasmi Dario ni mchezaji wa Singida na ana kandarasi ya miaka mitatu na yuko vizuri tu, jana alipata majeraha kidogo lakini madakatari wamethibitisha kwamba yuko sawasawa ataendelea na maandalizi.
“Niseme tu kwa sasa hakuna mlango wowote uliofunguliwa wa mchezaji wa Singida kwenda sehemu nyingine, lakini kama unavyofahamu soka ni biashara ndiyo maana Dario sasa yuko kwetu kwa sababu na sisi tulimnunua kutoka kwingine lakini pale tu milango inapofunguliwa na sasa hakuna kilichofunguliwa,” alisisitiza Ten.
Singida hata hivyo, hivi karibuni timu hiyo ilikubali kumuachia mshambuliaji wao mpya kutoka Mbeya Kwanza, Habibu Kyombo kwenda Simba baada ya makubaliano maalum.
Hilo pia limeunganishwa na tukio la awali la Singida United ilivyokubali kuwapa Yanga kiungo Feisal Salum ikiwa ni siku chache zimepita tangu wakamilishe usajili wa mchezaji huyo kutoka JKU ya Zanzibar msimu wa 2018/19.
Matukio hayo yote yamewafanya baadhi ya mashabiki kuamini kwamba hata kwa Dario jambo hilo linawezekana kutokea.
Soka Singida Big: Dario haendi Yanga
Singida Big: Dario haendi Yanga
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
