Na mwandishi wetu
Klabu ya Yanga imeingia mkataba wa miaka miwili na Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) wenye makubaliano ya kubadilishana huduma ambapo Yanga itapata punguzo la gharama za usafiri na kuitangaza ATCL kwenye safari zao.
Mbali na kuitangaza ATCL katika mkataba huo uliosainiwa leo Jumatano jijini Dar es Salaam, pia Yanga wataitangaza Tanzania ikiwa ndio lengo mama la mkataba huo kama ilivyoelezwa na Rais wa Yanga, Hersi Said.
“Leo Young Africans SC tumeingia ushirika na Shirika la Ndege la Air Tanzania ambapo tutaitangaza biashara ya ATCL. Ushirika huu unahusisha punguzo la bei kwenye safari zetu ambazo tutafanya na shirika hili. Hatuwezi kuona huduma ya Air Tanzania inafanyika bila sisi kuitangaza. Kufanya hivyo ni kuunga mkono juhudi za Serikali yetu pia.
“Tumesaini mkataba wa miaka miwili kuitangaza Air Tanzania katika kipindi chote hicho. Nasi kama Yanga tuna matumaini makubwa kuwa tutaendelea kunufaika na huduma bora za shirika hili kwa bei punguzo. Tunatambua mchango mkubwa wa ATCL kwa klabu yetu nasi tunao wajibu wa kuwaunga mkono,” alisema Said.
Naye Mtendaji Mkuu wa ATCL, Laudislaus Matindi alisema: “Tuna uhakika Young Africans SC watakwenda sehemu nyingi sana ndani ya bara la Afrika. Kwa mantiki hiyo itakuwa fursa kubwa kwetu kama shirika kutangaza utalii wa Tanzania kupitia Young Africans. Kwa kifupi the Wings of Kilimanjaro itapeperushwa kwa ukubwa wake zaidi ndani ya bara la Afrika na Young Africans SC.”